Ni huzuni Msimbazi, Singida BS yaitoa Simba FA

Muktasari:
- Ushindi kwa Singida BS umeifanya kulipa kisasi baada ya kuchapwa mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu, ikianza na kichapo cha bao 1-0, Desemba 28, 2024, kisha Mei 28, 2025, ikachapwa pia 1-0, huku ikifuta uwezekano wa kuwepo Dabi ya Kariakoo ya tatu kwa Yanga dhidi ya Simba baada ya kuchezwa Oktoba 19, 2024 na ile iliyopangwa kufanyika Juni 15, 2025, zikiwa ni za Ligi Kuu.
SINGIDA Black Stars imefuzu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya leo Jumamosi Mei 31, 2025 kuifunga Simba mabao 3-1, katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.
Ushindi kwa Singida BS umeifanya kulipa kisasi baada ya kuchapwa mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu, ikianza na kichapo cha bao 1-0, Desemba 28, 2024, kisha Mei 28, 2025, ikachapwa pia 1-0, huku ikifuta uwezekano wa kuwepo Dabi ya Kariakoo ya tatu kwa Yanga dhidi ya Simba baada ya kuchezwa Oktoba 19, 2024 na ile iliyopangwa kufanyika Juni 15, 2025, zikiwa ni za Ligi Kuu.
Mabao ya Singida BS yamefungwa na Jonathan Sowah dakika ya 17, baada ya kuwatoka mabeki wa Simba, huku la pili likifungwa na Emmanuel Keyekeh dakika ya 35 kufuatia kosa la kipa wa Simba, Ally Salim aliyepiga mpira mfupi na kumkuta mfungaji.
Salim alifanya kosa hilo ikiwa ni muda mchache tangu achukue nafasi ya Moussa Camara aliyeshindwa kuendelea na mechi dakika ya 27 baada ya kuumia, kabla ya Keyekeh tena kutupia bao lake la pili na la tatu kwa Singida BS dakika ya 48.

Keyekeh alifunga bao hilo kwa frii-kiki kali akiuzamisha mpira wavuni baada ya winga wa Singida BS, Edmund John kufanyiwa madhambi nje ya eneo la 18 na beki wa kulia wa Simba, David Kameta 'Duchu' na kupelekea maumivu ndani ya kikosi hicho.
Dakika ya 67, Jean Charles Ahoua akaifungia Simba bao la kufutia machozi, baada ya kupiga mpira wa frii-kii uliomshinda kipa wa Singida BS, Amas Obasogie na kuzama wavuni, ingawa haikubadilisha chochote na miamba hiyo kukubali kichapo hicho.
Singida BS ilianza michuano hiyo katika hatua ya 64, kwa kuifunga Magnet FC zamani Malimao ya Dar es Salaam, kisha hatua ya 32, ikakutana na mabingwa wa Mkoa wa Kagera, Leo Tena na kuichapa mabao 4-0 na kufuzu kibabe katika hatua ya 16, bora.
Hatua ya 16 bora, Singida BS ikakutana na KMC FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara na kuichapa bao 1-0, huku hatua ya robo fainali ikaichapa Kagera Sugar mabao 2-0 na kufuzu nusu fainali, kisha kuiondosha Simba kwa kuifunga 3-1 na kutinga fainali.

Ushindi huo wa Singida BS wa 3-1, unaifanya kuvunja rekodi ya Simba iliyodumu kwa takribani siku 573 kuanzia Novemba 5, 2023 hadi Mei 31, 2025 ambapo tangu mara ya mwisho kikosi hicho kilipochapwa 5-1 na watani zao wa jadi, Yanga katika mechi ya Dabi ya Kariakoo, hakijaruhusu zaidi ya mabao mawili kwenye mechi moja.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Novemba 5, 2023, bao pekee la Simba lilifungwa na Kibu Denis, huku yale ya Yanga yakifungwa na Kennedy Musonda, Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua na Maxi Mpia Nzengeli akifunga mawili.
Singida sasa inakwenda kukutana na Yanga katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA itakayochezwa kati ya Juni 26 hadi 28, mwaka huu kwenye uwanja ambao bado haujatangazwa.
Kitendo cha Simba kuondolewa katika michuano hiyo, kimeifanya kupoteza kombe lingine baada ya hivi karibuni kufungwa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane kwa jumla ya mabao 3-1.
Hivi sasa Simba inawania ubingwa wa Ligi Kuu Bara pekee, ikibakiza mechi tatu dhidi ya Yanga iliyopangwa kuchezwa Juni 15, 2025. Kisha dhidi ya KenGold (Juni 18) na Kagera Sugar (JUni 22).

Simba iliyopo nafasi ya pili na pointi 72 nyuma ya Yanga inayoongoza na pointi 73 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, huenda mechi ijayo ya Dabi ikatoa hatima ya kutwaa taji la ligi msimu huu, baada ya kulikosa kwa misimu mitatu mfululizo, likibebwa na Yanga.