Ngome yajipima kujiandaa mashindano ya Majeshi

Mtwara.  Timu ya soka ya Ngome imeimfunga mwenyeji wake Ndanda bao 2-0 katika mechi ya kirafiki iliyofanyika leo Februari 5, 2023 kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani hapa.

Bao la kwanza limefungwa na Juma Iddi katika dakika ya 14 huku Hamadi Mashinga akiiipatia kicheko cha pili timu hiyo katika dakika ya 32.

Kocha Mkuu wa timu ya  Ngome, Neveling Kanza ameiambia Mwanaspoti kuwa mchezo huo wa kirafiki ni katika kujipima nguvu kuelekea Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi  Tanzania (BAMMATA) inayotarajia kuanza Februari 9 hadi Februari 21, 2023.

Katibu Mkuu wa BAMMATA, Kanali Martin Msumari amesema kuwa mashindano  hayo yanashirikisha timu kutoka majeshi mbali mbali kutoka Bara na Visiwani Zanzibar ikiwemo Magereza, Polisi, Uhamiaji, Jeshi la Wananchi, JWTZ,  Jeshi la Kujenga Taifa, JKT, Zimamoto na vikosi vya Serikali ya Malpinduzi Zanzibar, SMZ.

Kanali Martin amewataka wakazi wa Mtwara kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo hiyo ambayo imedhamiria hasa kudumisha udugu na urafiki kwa vyombo vya ulinzi na usalama.  

Michezo itakayochezwa ni pamoja na soka, riadha, kulenga shabaha, kurusha vishale, ngumi, judo mpira wa mikono, mpira wa pete, wa wavu, na mingine mingi.