Ngoma awasaparaizi mashabiki Simba

Muktasari:
- Ngoma ameaga ikiwa siku chache tu, tangu Simba ilipopoteza pambano la dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga kwa mabao 2-0 na kuzima matumaini ya kubeba taji la Ligi Kuu.
SIKU chache baada ya kucheza mechi ya mwisho kwa msimu huu wa 2024-2025 wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga, kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma amewasapraizi mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwaaga rasmi leo kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Ngoma ameaga ikiwa siku chache tu, tangu Simba ilipopoteza pambano la dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga kwa mabao 2-0 na kuzima matumaini ya kubeba taji la Ligi Kuu.
Ameandika; "Habari za asubuhi nyote, ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru wote mlionifanya nijisikie kama nyumbani hapa Simba, nawashukuru sana Bwana Salum Try Again na Boss MO kwa kunileta hapa misimu miwili iliyopita.
"Shukrani kwa kocha, benchi la ufundi, na wachezaji wenzangu tuliogawana nao chumba cha kubadilishia nguo. Hatukuweza kufanikisha malengo yote tuliyopanga, lakini kumbukumbu zote zitabaki milele moyoni na akilini mwangu."
"Kwa mashabiki wa Simba, asanteni kwa sapoti yenu isiyoisha, msiwahi kuikata tamaa klabu yenu, nyakati nzuri zinakuja hasa mkiwa na kocha kama Fadlu, asanteni sana na nawatakia kila la heri katika maisha na msimu unaokuja."
Ngoma alijiunga na Simba misimu miwili iliyopita kupitia dirisha kubwa la msimu wa 2023-2024 akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan na tangu aitumikie timu hiyo amebeba nayo Ngao ya Jamii tu Agosti 13, 2023 ilipoifunga Yanga kwa penalti 3-1 baada ya suluhu ya dakika 90, jijini Tanga.
Lakini aliisaidia Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ikitolewa kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane, hatua ambayo kwa misimu takribani mitano timu hiyo iliishia robo fainali na katika Ligi Kuu msimu huu nyota huyo amefunga mabao manne, Simba ikimaliza ya pili.