Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndoa ya Mserbia, KenGold yafikia tamati

NDOA Pict

Muktasari:

  • Kocha huyo aliyejiunga na timu hiyo Januari 18, 2025, kwa lengo la kusaidiana na Omary Kapilima na Jumanne Challe, hadi ameondoka ameshindwa kuongoza benchi la ufundi kama kocha mkuu kwa mechi za Ligi Kuu kutokana na kukosa kibali cha kazi.

KLABU ya KenGold imefikia uamuzi wa kuachana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo raia wa Serbia, Vladislav Heric baada ya kikosi hicho cha Chunya mkoani Mbeya kushuka Ligi Kuu Bara kikiwa na mechi tatu mkononi za kuhitimisha msimu huu.

Kocha huyo aliyejiunga na timu hiyo Januari 18, 2025, kwa lengo la kusaidiana na Omary Kapilima na Jumanne Challe, hadi ameondoka ameshindwa kuongoza benchi la ufundi kama kocha mkuu kwa mechi za Ligi Kuu kutokana na kukosa kibali cha kazi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KenGold, Benson Mkocha alisema wamefikia makubaliano hayo ya kuvunja mkataba na kocha huyo, hivyo kikosi hicho kwa sasa kitaendelea kuongozwa na makocha, Omary Kapilima na Jumanne Challe.

"Baada ya timu kushuka tumefikia uamuzi huo kwa maslahi ya pande zote mbili, suala la Kapilima na Challe kuendelea nao hadi Championship kwa msimu ujao ni haraka sana kuzungumzia hilo, hivyo tusubiri tumalize kwanza msimu," amesema.

Mkocha amesema kitendo cha kushuka daraja kimewaumiza viongozi kutokana na jitihada kubwa walizozifanya hasa dirisha dogo la Januari kwa kusajili mastaa wakubwa, ingawa wamekubaliana na kilichotokea na wanakwenda kujipanga ili warejee upya.

Kikosi hicho kimeshuka daraja na msimu ujao kitashiriki Ligi ya Championship kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri hadi sasa, kikiburuza mkiani na pointi zake 16, baada ya kushinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 17 kati ya 27 iliyocheza.

Timu hiyo ilianza msimu na Kocha Fikiri Elias ingawa alijiuzulu kutokana na mwenendo mbaya Septemba 17, 2024, kisha baada ya hapo akaiongoza Jumanne Challe aliyeipandisha Ligi Kuu hadi Oktoba 22, 2024, alipoichukua Kapilima.

Heric kabla ya kutangazwa kuiongoza KenGold aliwahi kuzifundisha Club Africain ya Tunisia, Maritzburg United, Polokwane City, FC Cape Town, Chippa United za Afrika Kusini akisifika kwa uzoefu aliokuwa nao kutoka Serbia.

Kocha huyo aliyezaliwa Agosti 29, 1966, alianza kucheza mwaka 1976 akiwa na kikosi cha akademi ya FK Vojvodina's kisha soka lake la kulipwa alizitumikia timu mbalimbali zikiwemo za FK Proleter Novi Sad na FK Fruskogorac Novi Sad za Serbia.

Heric ambaye ni mzoefu wa Mpira wa Miguu akiwa na Shahada katika Chuo Kikuu cha Novi Sad huko kwao Serbia huku akipata UEFA 'A' License, aliacha kucheza soka la ushindani akiwa na miaka 21, baada ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.