Simba yaichapa JKT Tanzania, yatanguliza mguu mmoja Ligi ya Mabingwa

Muktasari:
- Kipindi cha kwanza Simba ilionekana kuhitaji bao la kuongoza ikiliandama lango la JKT Tanzania, kama sio umakini wa mabeki wa timu mwenyeji basi tungekuwa tunazungumza mengine.
BAO la kiungo Fabrice Ngoma alilofunga katika dakika za nyongeza kipindi cha kwanza, limetosha kuipa Simba ushindi wa 0-1 dhidi ya JK Tanzania na kujihakikishia nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ikifikisha pointi 63 ikiwafuata watani zao wa jadi, Yanga.
Kipindi cha kwanza Simba ilionekana kuhitaji bao la kuongoza ikiliandama lango la JKT Tanzania, kama sio umakini wa mabeki wa timu mwenyeji basi tungekuwa tunazungumza mengine.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar, JKT Tanzania iliingia na mfumo wa kujilinda zaidi ambapo hadi inafika dakika ya 45, ilifanikiwa kulinda vizuri lango lake lakini katika dakika saba za nyongeza, ilijikuta ikiruhusu bao hilo pekee.
Kabla ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilifanya mashambulizi kadhaa ambapo kona fupi iliyoanzishwa na Jean Charles Ahoua, pasi fupi ilimkuta Joshua Mutale aliyemuachia Steven Mukwala ambaye aliwapiga chenga mabeki wa JKT Tanzania na kupiga krosi iliyomaliziwa vizuri na Ngoma.
Ngoma ambaye alipumzishwa katika mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1, hilo linakuwa bao lake la nne msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara.
Kipindi cha pili kabla ya kuanza, JKT Tanzania ilifanya mabadiliko ya kumtoa Najim Magulu na kuingia Hassan Dillunga, ambapo timu hiyo ilionesha uhai ikitafuta bao la kusawazisha lakini uimara wa Simba haikuwa rahisi kwao kuambulia kitu.
Hata hivyo, Simba ilikuwa ikicheza kwa tahadhari kubwa sana kulinda bao hilo huku ikifanya mashambulizi kadhaa lakini kipa wa JKT Tanzania, Yacoub Mohammed alikuwa imara.
Simba katika kujiimarisha, ilifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji kwa nyakati tofauti ikiwatoa Steven Mukwala, Debora Mavambo, Jean Charles Ahoua, Joshua Mutale na Valentine Nouma, nafasi zao zikachukuliwa na Elie Mpanzu, Che Fondoh Malone, Leonel Ateba, Ladack Chasambi na Mohamed Hussein.
JKT Tanzania nayo ilimtoa Abrahim Seif akaingia Said Ndemla, Ramadhan Kichuya alimpisha Japhar Abdul, Edward Songo akichukua nafasi ya Hassan Mohammed.
Hicho ni kiporo cha pili kwa Simba ambapo imeshinda vyote, imebakiwa na viwili dhidi ya Pamba Jiji na KMC ili kuwa na michezo 26 sawa na vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga yenye pointi 70.
Kichapo hicho ni cha pili kwa JKT Tanzania msimu huu kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya Februari 13, mwaka huu kufungwa pia 0-1 dhidi ya Singida Black Stars. Nyumbani JKT Tanzania imecheza mechi 14, imepoteza mbili, sare nane na kushinda nne.
JKT Tanzania imeendelea kusalia nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 27, imebakiza mechi tatu kumaliza msimu huu.