Ndayiragije aiponza Geita Gold, yafungiwa

Ndayiragije aiponza Geita Gold, yafungiwa

SIKU chache tangu Biashara United kukutana na rungu na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa kufungiwa kusajili kwa madirisha mawili, nao Geita Gold yamewakuta kwa kuzuiwa kusajili hadi itakapomlipa aliyekuwa Kocha Mkuu wao, Etienne Ndayiragije.
Biashara ilipigwa rungu na Fifa majuzi kwa kukaidi agizo la kumlipa aliyekuwa mchezaji wao, Timoth Omwenga, lakini Geita iliyopo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na ikiisaka tiketi ya michuano ya kimataifa ya CAF imekumbana na adhabu hiyo kwa kushindwa kumlipa fidia kwa kumvunjia mkataba sambamba na malipo mengine  akiifundisha timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jioni hii (leo Ijumaa) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni kwamba kocha huyo wa zamani wa Mbao, KMC, Azam na Taifa Stars alifungua madai dhidi ya Geita akidai fidia ya kuvunjiwa mkataba na malipo yake mengine.
Iwapo itashindwa kumlipa kocha huyo suala hilo litawasilishwa katika Kamati ya Nidhamu ya FIFA kwa ajili ya hatua zaidi ya kinidhamu.
Ndayiragije alinyakuliwa na Geita mechi za awali za Ligi Kuu Bara ili kuchukua nafasi ya Fred Felix 'Minziro' aliyeipandisha timu hiyo, lakini baada ya kushindwa kuipa matokeo mazuri ilimtema na kumrudisha Minziro aliyeibeba hadi kuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tiketi ya CAF, huku straika wake, George Mpole akichuana na Fiston Mayele wa Yanga katika ufungaji mabao. Washambuliaji hao kila mmoja amefunga mabao 16 hadi sasa, ligi ikisaliwa na mechi za raundi mbili kabla ya kufikia tamati Juni 29.
TFF, linazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zinaingia na wachezaji pamoja na makocha kwani hiyo ni moja ya vigezo vya kupata leseni ikiwa ni utekelezaji wa Kanuni na Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations).