Nani zaidi ya Pacome, Chama gwiji aingilia

Muktasari:

  • Gwiji huyo amesema Pacome anatumia nguvu, anakaa na mpira mguuni na kabla ya kuupiga anakuwa amefanya uamuzi sahihi wa kutoupoteza.

STAA wa zamani wa Yanga, Idd Moshi, ameingia katika mjadala ambao umekuwa ukiendelea tangu msimu huu uanze kwa mashabiki kila mmoja akiwalinganisha kwa mtazamo wake viungo hodari nchini, Clatous Chama wa Simba na Pacome Zouzoua wa Yanga.

Viungo vipenzi vya mashabiki wa soka, Pacome na Chama, kila mmoja amefunga mabao saba kwenye Ligi Kuu Bara, na wote ni muhimu kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao.

Gwiji huyo amesema Pacome anatumia nguvu, anakaa na mpira mguuni na kabla ya kuupiga anakuwa amefanya uamuzi sahihi wa kutoupoteza.

"Kwa upande wa Chama anatumia akili kubwa anapokuwa na mpira na aina yake ya ufungaji ni ya kipekee, ana uwezo wa kuwachambua mabeki ikiwemo na kipa akafunga, lakini anachozidiwa na Pacome anaweza akafanya vitu vingi kama kutumia nguvu na uwezo wa kunyang'anya mpira ukiwa kwa mpinzani," amesema Moshi na kuongeza;

"Sina maana mbaya kwamba Chama ni mbaya, ila mpira ukiwa kwa mpinzani ni ngumu kuunyang'anya, hatumii nguvu, ila anaweza akapiga ambapo hukutarajia, ukidhani anatoa pasi kumbe anafunga mwenyewe."

ALIIFUNGA SIMBA AKITOKA KUOA
Katika dabi ya Agosti 5, 2000 Moshi ndiye aliyeifunga Simba mabao mawili Yanga ikiwafunga Wekundu wa Msimbazi 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) jijini Dar es Salaam, akiwa ametoka kwenye fungate baada ya kufunga ndoa na amesimulia tukio hilo.

"Harusi yangu ilikuwa siku mbili kabla ya mechi, ilifanyika mkoani kwetu Tabora, viongozi wa Yanga walinikatia tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi," amesema na kuongeza;

"Wengi wanajiuliza nilifanikiwaje, kwanza nilioa mwanamke anayeijua kazi yangu, hivyo alifahamu nikiwa na kazi mbele yangu anapaswa kufanya kitu gani, pia nilijituma ili ajivunie uwepo wangu uwanjani."

Kuhusu Dabi ya Aprili 20, amesema haitabiriki, anayejipanga vizuri ndiye anayewapa kicheko mashabiki wake, ingawa anaiona Yanga ina nafasi kubwa ya kushinda, kulingana na kikosi chao imara.