Namungo yaikomalia Azam FC

JITIHADA za Azam FC kumaliza msimu wakiwa nafasi ya pili zimeanza kufifia baada ya jana kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Namungo.

Mchezo huo mkali na wa kusisimua uliogubikwa na ushindani zaidi ulipigwa katika uwanja wa Majaliwa Mkoani Lindi na timu zote kutoka vichwa chini kwa kugawana pointi moja moja.

Endapo Azam FC ingepata ushindi katika mchezo huo ingejiweka pazuri kwani Yanga iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 67 baada ya kujitupa dimbani mara 31 huku wao wakicheza michezo 32 na kukusanya pointi 64.

Katika mchezo huo timu zote zilikosa nafasi mnamo dakika ya 14 Sey alikosa nafasi ya kufunga baada ya shambulizi lake kuishia nje, dakika 18 Wadada nusura ajifunge baada ya kutaka kupiga mpira mbele na kurudi nyuma huku mlinda mlango akiwa makini na kuudaka.

Dakika ya 20 Lyanga anakosa nafasi na mabeki wakahokoa, huku pia umakini ukikosa kwa Braison dakika 23 Braison shuti lake liliambaa nje ya lango, dakika ya 36 Braison alipewa kadi ya njano kwa kumchezea madhambi Haruna Shamte.

Upinzani ulizidi zaidi Sey akikosa nafasi ya kufunga dakika 38 baada ya kushindwa kuitendea haki pasi ya Kikoti, dakika ya 45 Mudathir alikosa nafasi na mpira kuokolewa na mabeki wa Namungo na kupelekea mapumziko wote kutoka vichwa chini.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa huku Lyanga akikosa na dakika ya 56 Mlinda mlango wa Azam alipewa kadi ya njano baada ya kuonekana kaumia na kutibiwa baadae kunyanyuka na kutembea lakini dakika chache baadae aliomba kuondolewa na nafasi yake kutwaliwa na Wilbol Maseke.

Dakika ya 68 Nado alikosa nafasi baada ya Jaffar kuokoa na kumgonga Jonathan katika harakati za kutoa mpira katika eneo la hatari huku dakika ya 90 Kikoti shuti kali likipanguliwa na mlinda mlango na kupelekea mchezo huo kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Kocha Msaidizi wa Azam Vivier Bahati alisema, mechi ilikuwa ngumu na yenye ushindani kila timu imepambana kupata matokeo lakini ndio mchezo na kusema hivi sasa anaitizama mechi ya FA dhidi ya Simba Juni 26 akikiri ni mechi ngumu kwa pande zote mbili.

Kwa upande wa Kocha wa Namungo Hemed Morocco alisema,  "Ilikuwa mechi nzuri kwetu na hata Azam, kilichotokea ni matokeo ya mpira,"

Alisema, kwa sasa anatizama mechi mbili zilizosalia katika Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting pamoja na Simba akiamini atapambana kupata matokeo

KIKOSI NAMUNGO
Jonathan Nahimana, Haruna Shamte, Jaffar Mohamed, Kalos Protus, Hamis Fakh, Hamis Halifa, Stephen Sey, Fred Tangalo, Ibrahim Abdallah/Kwizera, Lucas Kikosi pamoja na Abeid Athman.


KIKOSI AZAM
Mathias Kigonya, Nicolaus Wadada, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Agrey Morice, Braison Nkulula/Tigere, Idd Nado, Salum Abubakar, Mpiana Platini, Mudathir Yahya na Ayoub Lyanga