Namungo yabeba kisasi cha Yanga

Dar es Salaam. Namungo FC itakuwa na kibarua cha kulipa ama kupunguza deni sugu la Yanga lililodumu kwa miaka 22 wakati watakapokabiliana na miamba ya Morocco, Raja Casablanca leo ugenini huko Morocco kuanzia saa 1.00 usiku kwa muda wa Tanzania.

Septemba 18, 1998 katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilipokea kichapo kizito cha mabao 6-0 pindi walipokabiliana na Raja Casablanca kwenye Uwanja wa Mohamed V uliopo jijini humo kipigo ambacho hadi leo kinabakia kuwa kikubwa zaidi kwa timu ya Tanzania kukipata katika mechi moja ya hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.

Baada ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kwa kutopoteza mechi yoyote ya ugenini, Namungo leo wana dakika 90 za kufanya maajabu mbele ya Raja Casablanca ugenini na kufuta machungu ya ndugu zao Yanga waliyoyapata miaka mingi iliyopita.

Ni mchezo mgumu kwa Namungo FC ukizingatia ubora wa kikosi, historia na uwekezaji mkubwa wa fedha wa Raja Casablanca ukilinganisha na wawakilishi hao wa Tanzania ambao pengine ukizidisha bajeti yao mara 20 au zaidi ndio unapata ile ya wapinzani wao.

Kihistoria, Raja Casablanca ina uzoefu wa kutosha na mafanikio makubwa katika mashindano ya klabu Afrika ambayo imetwaa mataji manne kwa maana matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika na moja la Shirikisho Afrika

Hiyo iko kinyume na Namungo FC ambayo ndio inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya klabu Afrika kama ilivyo kwa hatua ya makundi baada ya kuzitupa nje timu za Al Rabita, Al Hilal Obeid pamoja na Primiero De Agosto ya Angola.