Kagere apewa mchongo mpya

JINAMIZI la kukosa penalti linalomsakama straika wa Simba, Meddie Kagere limetafutiwa suluhisho la namna ya kuondoka na hali hiyo, kisha kuwa fundi wa kuzipiga zile za video.

Kitendo cha Kagere kukosa penalti mara tano tangu ajiunge na timu hiyo msimu wa 2018/2021 ni kama kinawanyima raha mashabiki wake inapofikia hatua hiyo. Pia kuwapa nguvu makipa kumtoa mchezoni.

Mara ya mwisho Kagere kukosa penalti ilikuwa Februari, mwishoni wakati Simba ilipocheza na African Lyon, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Wachezaji wa zamani, makocha na wataalamu wa saikolojia wamempa njia ya jinsi ya kuondoka na changamoto hiyo.


SIMBA vs Lyon -ASFC

Hivi karibuni wakati Simba inacheza mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ya mtoano dhidi ya African Lyon, Kagere alikosa penalti. Wakati anajiandaa kwenda kuipiga dakika ya 22, mchongo wa pasi yake ulienda pembeni ya goli la mlinda mlango wa Lyon. Penalti hiyo ilitokana na kuchezewa rafu Perfect Chikwende na mabeki wa Lyon, wakati anawapiga chenga ndani ya 18 ya lango lao.


SIMBA vs YANGA - MAPINDUZI

Simba na Yanga zilicheza fainali za Kombe la Mapinduzi 2021, lakini dakika 90 hakukuwepo mbabe na ilibidi iingie hatua ya penalti, ambapo Francis Kahata alitangulia kupiga ya kwanza akapata, ikafuata kwa upande wa Wanajangwani ikachongwa na Tuisila Kisinda naye akatikisa nyavu alizokuwa akizilinda Beno Kakolanya.

Penalti ya pili Simba ilipigwa na Kagere, lakini bahati mbaya mpira ulikwenda kugonga ukuta wa goli la mlinda mlango Farouk Shikalo, hiyo ikawa penalti ya pili kuikosa staa huyo kwenye michuano ya Mapinduzi.

Penalti ya kwanza Kagere alikosa dhidi ya Azam katika fainali za Kombe la Mapinduzi 2019 ambapo alipiga ya tano ambayo ilidakwa na kipa Razack Abarola, licha ya kwamba Simba ndio ilichukua taji hilo baada ya Kakolanya kudaka penalti ya kipa wa Azam ambaye aliamua kupiga mwenyewe.


SIMBA vs BIASHARA UNITED-VPL

Wakati Kagere anakwenda kupiga penalti dakika ya 26 ni kama alikuwa anasomwa akili na picha ya mwili vinaongea nini na kipa wa Biashara United, Daniel Mgore, ambaye baada ya kupigwa shuti alilipokea mikono miwili kama vile alikuwa analisubiri kwa hamu. Mchezo huo ulipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa msimu 2019/20.


KMC vs SIMBA - VPL

Mechi ya KMC na Simba iliyopigwa Aprili 25, 2019 mjini Mwanza, Kagere alikosa penalti baada ya kupiga shuti lililoangukia mikononi mwa kipa wa Jonathan Nahimana.


NENO LA WADAU

Kocha wa Pan African, Godian Mapango ambaye aliichezea timu hiyo na Yanga zamani anamshauri Kagere kujiamini na kuchukulia kuwa hilo ni jukumu lake la kila siku, bila kujali kuzomewa na mashabiki.

“Kwanza lazima uwe imara ukichezea Simba na Yanga zenye mashabiki lukuki, pamoja na kwamba Kagere kakosa mara nyingi (penalti) isimsumbua nakuona hastahili kupiga, lakini pia liwe zoezi analolifanyia kazi sana mazoezini. Atakaa sawa na kuwa mfungaji mzuri na jambo la msingi zaidi hata mastaa wakubwa Ulaya wanakosa,” anasema.

Staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel anasema hakuna fundi wala dhaifu wa penalti, lakini jambo kubwa alilopaswa kulifanya Kagere ni kujipa ujasiri na kuona anaweza kufanya vyema kama anavyofanya anapofunga mabao ya kawaida.

“Ndio maana hata Ulaya wanakosa, mbali na hilo kila jambo linahitaji kulifanyia mazoezi zaidi ili kufanya kwa kujiamini, naamini hata makipa wanaodaka wanafanya zaidi mazoezi,” anasema.

Naye straika wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi anasema ni afadhali Kagere anakosa penalti lakini hazijamtoa mchezoni, tofauti na yeye yaliyomkuta 2014 alipokosa dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanya timu hiyo ienguliwe hatua ya makundi.

“Kagere asife moyo, lakini awe anafanya mazoezi ya kupiga penalti sana wakati wa mazoezi na aendelee kupiga mara kwa mara ili kujijengea kujiamini, lakini kocha wake pia anatakiwa amtie moyo na kumuonyesha anamwamini.”


MWANASAIKOLOJIA

Mtaalamu wa saikolojia, Charles Nduku anamsaidia Kagere kumjenga akisema kwamba anatakiwa kujikubali na kujiamini kwamba anaweza kufunga na kuondoa kuyapa nafasi makosa ya nyuma.

“Ipo hivi, mtu yeyote anapokosea jambo, anapopewa nafasi nyingine anakuwa na mambo mawili kama hatapania basi atajawa na hofu.

Kagere anapokwenda kupiga penalti ndani ya kichwa chake asiwaze mashabiki wanasema nini juu yake, wala makipa wanamuondoaje kwenye mchezo, jambo la mwisho ni kocha wake kuendelea kumpa nafasi kwa kumwamini,” anasema.