Namungo yaanza vibaya MAkundi, yalala Morocco

CASABLANCA, MOROCCO


PENALTI ya dakika ya 54 iliyopigwa na Soufiane Rahimi wa Raja Casablanca, imeizamisha Namungo FC katika mechi yake ya kwanza ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mjini Casablanca.

Namungo inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza na kutinga makundi iliwabana wenyeji kwenye pambano kali lililopigwa katika Uwanja wa Mohamed V na kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa bila kufungana.

Hata hivyo, kipindi cha pili kilipoanza, wenyeji waliliandama lango la Namungo lililokuwa chini ya kipa Jonathan Nahimana na kujikuta mabeki wa ‘Wauaji wa Kusini’ hao kufanya madhambi yaliyowapa penalti Raja.

Dakika chache baadaye beki Haruna Shamte alijikuta akilimwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kuifanya Namungo icheze pungufu kwa dakika 24 zilizosalia za mchezo huo.

Licha ya kipigo hicho, lakini Namungo inayonolewa na Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ ilionyesha soka tamu na kukataa kuaibishwa kama Yanga iliyopigwa 6-0 na Raja iliposhiriki mara ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 1998.

Kwa matokeo hayo yameifanya Namungo kushika nafasi ya tatu baada ya Nkana FC ya Zambia kupoteza ugenini nchini Misri kwa mabao 2-0 mbele ya wenyeji wao Pyramids.

Wamisri hao ndio watakaocheza na Namungo FC katika mechi inayofuata kwa wawakilishi hao wa Tanzania, mchezo utakaopigwa Jumatano ijayo kwenyer Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.