Namungo: Wasudan hawachomoki nyumbani

Namungo: Wasudan hawachomoki nyumbani

Muktasari:

Hii ni mara ya kwanza Namungo inashiriki mashindano ya kimataifa na ilipata nafasi hiyo baada ya kuibuka washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho (FA).
 

KIUNGO wa Namungo FC, Lucas Kikoti amekiri wachezaji wote wa timu hiyo wako vizuri kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Al Rabita ya Sudan.

Namungo itaikaribisha Al Rabita katika mchezo wa hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika kesho Jumamosi Novemba 28 kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Kikoti amesema maandalizi yote yamekamilika na wachezaji wote wana ari kubwa ya kufanya maajabu katika mchezo huo na kupata ushindi.

"Wote tuko vizuri, kila mchezaji ana ari kubwa kuelekea mchezo huo kwa sababu tunataka kushinda kwa mabao mengi nyumbani ili itupe kazi rahisi tutakapokwenda ugenini.

"Tunajua sisi ni wageni katika mashindano haya lakini hatuna hofu kwani ni kama wanajeshi hatuogopi adui hivyo tutapambana kuhakikisha tunashinda huo mchezo licha ya kwamba tutaingia kwa tahadhari kwani hatuwajui vizuri wapinzani wetu', amesema Kikosi.

Kikoti amewaomba mashabiki wa soka kwenda uwanjani kwa wingi kuwapa sapoti na kutanguliza utaifa mbele.

"Tunawaomba mashabiki bila kujali itikadi za klabu zao waje kwa wingi uwanjani kutusapoti  kwani ujio wao utatupa hamasa sisi kama wachezaji kujituma zaidi uwanjani na kufanya vizuri" amesema Kikoti.

Na OLIVER ALBERT