Nabi: Tutafanyia kazi makosa

Tuesday May 10 2022
nabi pic
By Khatimu Naheka

Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi ameungana na mashabiki wa timu hiyo kuumizwa na matokeo ya sare tatu za mfululizo lakini akasema ni hatua mbaya kwa wachezaji wake kushambuliwa.

Nabi amesema hakuna ambaye amefurahia matokeo hayo lakini bado wana nafasi ya kurudi katika ubora wao wa ushindi kama awali.

Kocha huyo ambaye amerejea kwenye benchi baada ya kumaliza adhabu ya kusimamishwa mechi tatu, amesema anawapa pole mashabiki wao na watafanya juhudi kubwa za kufuta matokeo hayo kuanzia mechi ijayo.

Yanga itarejea uwanjani Mei 15 wakiwafuata ugenini Dodoma Jiji, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

"Hata mimi ningekuwa shabiki ningeumia, wanastahili ushindi lakini kuna wakati soka huwa na matokeo ya kikatili kama hivi, timu haikucheza vibaya lakini kitu kibaya ni kwamba hatukutumia nafasi tulizotengeneza," amesema Nabi.

"Bado naamini tuna wachezaji bora ambao wanatambua wapi tumekosea, tumewaambia wapumzike leo na kesho turudi kazini, mimi naamini kazi ninayofanya na wasaidizi wangu pamoja na wachezaji itabadilisha hali hii.

Advertisement

Nabi ameongeza kuwa katika mechi saba zilizobaki bado Yanga ina nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa ingawa amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanatuliza presha na kurudi katika njia ya ushindi.

" Tumebakiza mechi saba ukiniuliza timu gani ina nafasi ya kuwa bingwa nitakujibu haraka Yanga, kitu kilichotuangusha jana nadhani kuna presha iliwaingia wachezaji.

"Tutarudi kazini na kuzungumza nao, na kufanyia kazi makosa ambayo tuliyaona, mashabiki warudi kuwa sehemu ya timu, tunatakiwa kuendeleza umoja wetu, tutarudi kwa nguvu kuwafurahisha."

Yanga imetoa suluhu tatu za mfululizo katika jumla ya dakika 270 dhidi ya Simba, Ruvu na Tanzania Prisons.

Advertisement