Nabi, Robertinho walivyoitabiri Dabi

Muktasari:

  • Kuelekea katika mtanange huo wa Jumamosi  wenye presha kubwa kocha huyo alisema ijapo anatingwa sana na majukumu na ugumu wa Ligi ya Morocco akiwa na kikosi chake kipya cha FAR Rabat lakini akipata nafasi huwa anawatazama Yanga.

JUMAMOSI ni Dabi. Yanga ambayo ndio wenyeji wa mchezo huu,misimu miwili nyuma ilikuwa ikiongozwa na kocha Nasreddine Nabi kabla ya kuja kwa Miguel Gamondi na kuacha rekodi kubwa ya kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita na kutwaa taji la FA na Ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Kuelekea katika mtanange huo wa Jumamosi  wenye presha kubwa kocha huyo alisema ijapo anatingwa sana na majukumu na ugumu wa Ligi ya Morocco akiwa na kikosi chake kipya cha FAR Rabat lakini akipata nafasi huwa anawatazama Yanga.

Alieleza kuwa ameziangalia mechi chache za kimataifa na kwa uzoefu wake kwa muda ambao alifanya kazi hapa Tanzania, mechi dhidi ya Simba na Yanga siku zote huwa na presha kubwa kwa kila upande.

Aidha alisema kuwa Yanga inaonekana kuwa vizuri ukilinganisha na matokeo ya mechi inazoshinda, na kwa upande wa pili Simba inaonekana kuyumba lakini hizi mechi kuna wakati haziangalii matokeo ya nyuma na inaweza kuja na matokeo ya tofauti.

“Yanga hawatakiwi kuidharau Simba, kwani inahasira na matokeo ambayo wanayapata ni rahisi kwao (Simba) kuja na nidhamu kubwa ya kuwazuia Yanga na wakifanikiwa inaweza kuwa mechi ngumu kwa Yanga.

Faida iliyonayo timu yangu cha zamani ni kikosi ambacho kinaweza kuamua matokeo chenyewe, namuheshimu sana kocha wao Miguel Gamondi ameonyesha ni kocha mzuri tangu achukue nafasi yangu,”aliongeza kuwa;

“Simba pia ina kocha mzuri Benchikha anajua kucheza mechi kubwa, nadhani wachezaji wenyewe wataamua mchezo kulingana na hesabu za makocha wao,itakuwa mechi ngumu kwa timu zote lakini ni mechi ambayo itazalisha mabao,”alisema Nabi ambaye sasa yuko na FAR Rabat ya Morocco.

Kocha Oliviera Robertinho, ambaye alitimuliwa baada ya kipigo mabao 5-1 walichokipata katika mchezo uliopita alisema, siku zote hakuna dabi rahisi wakati mwingine inaweza kuja na matokeo ya kushangaza.

Aidha alisema anawajua wachezaji wa Simba kama watawekwa vizuri kisaikolojia lakini pia benchi lao la ufundi likaja na mpango mzuri wa mechi kulingana na ubora wa wapinzani wao wanaweza kufanya vizuri na pengine hata tofauti na watu wanavyofikiri.

“Simba ina wachezaji wenye mioyo migumu kama Kibu, Ngoma, Chama, Saido, Inonga, Tshabalala,Che Malone, Kapombe,Kanoute hawa ni baadhi ya  wachezaji wakubwa wanaojua maana ya mechi kama hii kwa klabu.

Yanga ina timu nzuri ndio maana wanapata matokeo mazuri kuliko Simba, ni wazi itakuwa mechi ngumu kwani watakuja na morali kwamba walishinda mechi yao ya mwisho ya Ligi lakini pia mechi yao ya mwisho dhidi ya Simba,”alisema Robertiho.

Watani hao wa Jadi watakutana Ijumaa,Aprili 20 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa,   ikiwa ni mara yao ya pili kukutana msimu huu kwa ratiba ya ligi,huku Simba ambae ndie mgeni wa mchezo huo akiingia akiwa na rekodi mbaya ya kupigwa mabao 5-1 katika mchezo uliopita.