Nabi apanga silaha nzito, amnoa Mayele kuiua Azam!

Sunday October 24 2021
nabi silaha pic
By Charity James

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi mjanja sana. Baada ya kuona kazi kubwa aliyoipata mbele ya KMC na kutoka na ushindi wa mabao 2-0 mjini Songea, Ruvuma, ameamua kulipanga upya jeshi lake kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Azam akiamini utakuwa mgumu zaidi kuliko mechi zilizopita.

Yanga ndio vinara wa ligi hiyo kwa sasa wakiwa na pointi 9 kutokana na michezo mitatu waliyocheza na kushinda yote na mchezo ujao watavaana na Azam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa mechi itakayopigwa Oktoba 30 na Kocha Nabi anataka kuendeleza rekodi yake ya kushinda kwa asilimia 100.

Kocha huyo mwenye uraia pacha wa nchi za Ubelgiji na Tunisia, baada ya kuwapa mapumziko vijana wake, jana asubuhi ameanza kuwapika upya kwa kuwapigisha tizi la maana kwenye kambi yao iliyopo Avic Kigamboni, licha ya kuwakosa baadhi ya nyota wake walio majeruhi akiwamo Dickson Ambundo.

Katika mazoezi ya jana, Nabi alikomalia washambuliaji wake, wakiongozwa na Fiston Mayele na Heritier Makambo, ikiwa ni dalili kwamba anataka kushinda kwa idadi kubwa zaidi dhidi ya Azam waliopo Misri kwa sasa wakiliwakilisha taifa kwenye mechi za kimataifa za CAF.

Nabi amekuwa akiwapa mbinu nyota wake hao, huku akikazania namna ya kufunga mabao na katika kuona vijana wake wameiva kwa kiasi gani amewaomba mabosi wake mechi mbili za kirafiki fasta kabla ya kuwavaa Azam wikiendi ijayo.

Yanga imefunga mabao manne hadi sasa katika mechi zao tatu za ligi, ikiifumua Kagera Sugar na Geita Gold kila moja kwa bao 1-0 kabla ya kuifanyizia KMC kwa kuilaza 2-0 na inaelezwa utamu huo wa mabao umemnogea Nabi na sasa anataka kuona timu yake ikishinda mabao zaidi ili kufikia malengo yao.

Advertisement

Kwa misimu minne sasa, Yanga imekuwa ikisotea ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya watani wao Simba ambao kesho wana jukumu la kimataifa dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambako vijana wa Jangwani waliing’olewa katika raundi ya awali na Rivers United ya Nigeria.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ni kwamba benchi la Yanga linaheshimu kila mpinzani wao katika ligi na benchi lao limekuwa makini ndio maana limewarejesha mastaa wao kambini na kuwapigisha tizi la maana ili kuwaimarisha ili kupata matokeo mazuri.

“Kwa leo (jana) tumeanza mazoezi saa 3 na kutumia saa 2 kwa wachezaji kukimbia kabla ya kuchezea mpira na Nabi amekuwa akisisitiza kwenye ufundi wa kuona washambuliaji wakitumia nafasi na kufunga,” alisema.

“Baada ya hapo yalifuata mazoezi ya kuchezea mpira na baadaye kocha Nabi aligawa timu ambazo zilichuana lengo likiwa ni kufunga.

“Jambo zuri kwenye mazoezi hayo, Kocha Nabi hakuzingatia washambuliaji pekee tu katika kufunga bali kwa kila mchezaji aliyepata nafasi ya kufanya mazoezi alifanya kama alivyoelekezwa na walikuwa wanafanya hivyo kwa kufunga kwa mashuti ya mbali, kitu kinachovutia tukijiandaa dhidi ya Azam.”


MUSTAFA,

AMBUNDO BADO

Akizungumzia nyota ambao walishindwa kufanya mazoezi na wenzao, Bumbuli alisema Dickson Ambundo, Yassin Mustafa na Balama Mapinduzi bado wapo chini ya uangalizi na kocha wa viungo.

“Ambundo aliruhusiwa na kocha kwenda kwenda kwao ili kujiangalizia tatizo la mkono ambalo linamsumbua, Yassin na Balama wanaendelea kufanya mazoezi ya peke yao ili kurudi taratibu kwenye hali zao kabla hawajaanza kufanyishwa mazoezi magumu,” alisema na kuongeza Jumatatu Yanga itacheza mechi moja ya kirafiki bila kuitaja jina la timu ikiwa ni sehemu ya kutesti mitambo yao.


RATIBA

Ligi Kuu Bara

Okt 30, 2021

Yanga v Azam

Saa 1:00 usiku

Benjamin Mkapa

Advertisement