Nabi aipa Yanga mbinu za kuiua Mamelodi Dar

KIKOSI cha Yanga kinajiandaa kushuka uwanjani kesho Jumamosi kukabiliana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huku kocha wa zamani wa timu hiyo, Nasreddine Nabi akiitabiria kupata matokeo mazuri nyumbani sambamba na kuwapa mbinu za ushindi mbele ya Wasauzi.

Yanga itashuka kesho kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Mamelodi ilitua usiku wa jana nchini kwa ajili ya mchezo huo huku ikiwa imebeba kila kitu kukwepa kile kinachoelezwa ni hujuma dhidi ya wenyeji wao.

Hii ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya awali kuvaana katika mechi mbili za raundi ya pili kwa msimu wa 2001, ambapo Mamelodi ilishinda nyumbani mabao 3-2 na kutoka sare ya 3-3 ugenini na kuing'oa Yanga hatua hiyo.

Safari hii timu hizo zinakutana katika robo fainali baada ya Mamelodi kuongoza Kundi A mbele ya TP Mazembe ya DR Congo na Yanga kumaliza nafasi ya pili katika Kundi D nyuma ya watetezi Al Ahly ya Misri inayoshuka uwanjani usiku wa leo kuvaana na Simba katika mchezo mwingine wa robo fainali.

Akizungumzia mchezo huo wa kesho, Nabi ameliambia Mwanaspoti uwezekano wa Yanga kushinda nyumbani ni mubwa iwapo kama itaamua kucheza kwa nidhamu na kutumia nafasi inazozitengeneza, akisisitiza ni kweli Mamelodi ni wazuri, lakini wanafungika pia.

"Nawatakia kila la kheri Yanga, najua wana kikosi na benchi la ufundi bora, ikiwemo kocha Miguel Gamondi, naamini watafika mbali  na kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita iliyopita," amesema Nabi aliyeifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kulikosa tajio hilo kiduchu mbele ya USM Alger ya Algeria iliyobebwa na kanuni ya faida ya mabao ya ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni sare ya 2-2, Yanga ikifungwa 2-1 nyumbani na kushinda 1-0 ugenini.

"Jambo moja la muhimu ni kwamba wawalazimishe wapinzani wao kufanya makosa ili wapate nafasi ya kuwaadhibu, kwani mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, lakini yenyewe icheze kwa nidhamu na kutumia kila nafasi wanayoitengeneza, kisha ijipange kwa mechi ya marudiano," amesema Nabi anayeinoa Far Rabat ya Morocco inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo 'Botola Pro'.