Nabi: Aah wapi!

WAKATI huko Msimbazi, mashabiki wake wamekuwa wakitembea vifua mbele wakitamba kwamba keshokutwa, lazima wamtafune mtu watakapokutana na watani wao wa jadi, Yanga, lakini Kocha Mkuu wa Jangwani, Nasreddine Nabi ni kama amewaambia ‘aah Wapi’ baada ya kuwapanga vyema vijana wake mazoezini, huku akiwataja baadhi ya nyota wa Simba wa kuthibitiwa Kwa Mkapa.

Yanga imeendelea na mazoezi ya kibabe kuelekea Kariakoo Derby dhidi ya Simba na shoo nzima inasimamiwa na Nabi, lakini katika kuhakikisha vijana wake wanatambua jinsi ya kuzingatia maelekezo yake amekuwa akiwataja baadhi ya nyota wa Wekundu hao mazoezini.

Kwenye ratiba ya mazoezi ya Yanga muda pekee unaopotea ni ule wa baadhi yao kunywa maji kwa wale ambao hawako katika ibada ya Mfungo wa Ramadhani, lakini kinyume na hapo ni kazi ya kukaba na kushambulia.

Mazoezi ya juzi pale Avic, Kigamboni Kocha Nabi ameonekana kukomaa na nidhamu ya ukabaji ambapo amekuwa akiwapa mbinu mabeki wake wa pembeni mbinu za kuwazuia viungo wa Simba, Luis Miquissone na Clatous Chama.

Iko hivi. Nabi kila alipokuwa akiona beki wake anakosea kufanya kile anachotaka, alikuwa akisimamisha mazoezi huku akiwaambia kama akifanya kosa hilo, basi Chama au Luis watapitia upande huu.

Kwenda sambamba na hilo, Nabi amekuwa akiwapa akili ya jinsi ya kuwazuia viungo hao huku wachezaji hao hasa mabeki wa pembeni nao wakipambana kurekebisha.


WASHAMBULIAJI MABAO

Mbali na mabeki hao pia Nabi alikuwa akikomaa na washambuliaji wake ambapo kila walipofika eneo la hatari alitaka kuona mabao yanafungwa lakini viungo nao wanatoa pasi zilizo sahihi.

Eneo hilo alikuwa akitaka kuona kila mshambuliaji anakuwa na utulivu katika kutumia nafasi ambapo eneo la kiungo pia akitaka kuona pasi za haraka zinapigwa kuweza kukamilisha mashambulizi.

Kuonyesha kocha huyo raia wa Tunisia anataka usikivu ili ufanisi upatikane, nusura atibuane na Ditram Nchimbi ambaye alikuwa akiongea na wenzake wakati kocha huyo akitoa maelekezo.


CARLINHOS AZUA HOFU

Katika mazoezi hayo ya juzi yaliyofanyika kwa muda wa saa mbili kama kuna staa atakayewashtua mashabiki wa Yanga kuelekea mchezo huo basi ni Carlos Stenio Fernandes Guimarães do Carmo ‘Carlinhos’ ambaye alikuwa nje akifuatilia mazoezi hayo.

Carlinhos bado hajawa sawa baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Prisons huku habari njema ni kurejea kwa Tuisila Kisinda ambaye anasubiri mchezo tu akiwa na kasi yake ileile.