MZUNGU WA INGWE ASEMA TIMU BADO SANA

LICHA ya ushindi mnene wa magoli sita mtungi dhidi ya Tikki FC inayoshiriki divisheni ya pili kwenye uwaniaji wa kombe la Betway Cup wikendi, kocha mpya wa AFC leopards Mbelgiji Patrick Aussems kasema kuwa kikosi chake bado hakijaiva. Mzungu huyo kasisitiza Ingwe haipo kabisa katika kile kiwango anachokusudia.
Kulingana nae, kwa siku chache hizo alizokaa na timu hiyo, kagunduan bado wapo chini kinoma kiviwango na kusisitiza kwamba wanayo kazi nyingi ya kufanya kabla ya kufikia levo anazozitaka.
“Kifundi na kimbinu nimegundua kuwa tuna kazi nyingi ya kufanya. Wajua kila kocha mpya huja na filosofia yake na wakati mwingine huwachukua wachezaji muda kabla waielewe. Nimeshafanya vikao kadhaa vya mazoezi na nimegundua kuna mapungufu makubwa sana kwenye ufundi na mbinu. Hapa ndipo tukapoanzia.” Aussems kasema.
Kocha huyo anasema mpira anaoutaka kuona Ingwe wakicheza ni ule ambao mitaani huitwa ‘porno-soccer’. Ni soka ya kugusa kugusa mpira kwa pasi fupi fupi tena za haraka kwenda mbele huku mashambulizi yakipangwa kutoka nyuma.
Ni tofauti kabisa na staili yake kocha Antony ‘Modo’ Kimani aliyependeleza zaidi mtindo wa counter attack. Aussems anasema staili yake ya uchezaji itasaidia sana kumaliza udhaifu kwenye safu ya kati ambao ulishuhudiwa kwenye Mashemeji Derby, mopja ya mechi ngumu walizoshiriki mpaka sasa msimu huu.
Safu ya kati ya Igwe ilikuwa imekufa na mpira haikuwa ikifika mbele. Mara si moja straika Elvis Rupia alilazimika kurudi hadi mid kusaka mpira. Mpira mwingi wa Ingwe kwenye mechi hiyo ulitokea pembeni mwa uwanja huku ukiwacha shimo katikati na kuwaruhusu viungo wa Gor hasa Kenneth Muguna kuwang’aria.
Ubishi walioupata kutoka kwa Gor ulikuwa tofauti kabisa na Tikki waliotokea kuwa mteremko mbele ya Ingwe na kuwaruhusu kutawala mchezo mwanzo mwisho huku wakiwafunga magoli kiholela.