MZEE WA KALIUA: Kuna maisha baada ya 'Derby'

Muktasari:

  • Kwa wenzetu mara nyingi mtu mwenye timu bora hushinda, lakini Tanzania, Dabi ya Kariakoo usimalize maneno. Weka akiba kuna maisha baada ya tarehe 20 Aprili. Hakuna watu wanasubiri mechi ya Dabi ya Kariakoo kama mashabiki na wapenzi wa Yanga.

Nimewahi kuona Simba mbovu ikishinda mbele ya Yanga bora. Sio mara moja. Sio mara mbili. Nimewahi kuona Yanga mbovu ikishinda dhidi ya Simba bora. Sio mara moja. Sio mara mbili. Kariakoo Dabi sio ya kumaliza maneno. Ni mechi ya kuweka akiba. Unaweza kuumbuka. Unaweza kesho kushindwa kuwatazama watu usoni. Ni miongoni mwa vitu vya ajabu kwenye soka letu.

Kwa wenzetu mara nyingi mtu mwenye timu bora hushinda, lakini Tanzania, Dabi ya Kariakoo usimalize maneno. Weka akiba kuna maisha baada ya tarehe 20 Aprili. Hakuna watu wanasubiri mechi ya Dabi ya Kariakoo kama mashabiki na wapenzi wa Yanga. Kwanza wana kumbukumbu ya kuwafunga Simba mabao 5-1 kwa Mkapa mechi ya mkondo wa kwanza msimu huu. Pili, wameendelea kuwa bora ndani ya ligi huku Simba wakisuasua. Tayari wamesikika mashabiki wengi wa Simba kuonekana kuikatia tamaa timu yao.

Simba iko kwenye wakati ngumu ndani ya dimba. Simba imepoteza mechi nyingi hivi karibuni. Simba ni kama inajikokota lakini usiseme maneno ukamaliza. Weka akiba, Dabi ya Kariakoo ni habari nyingine kabisa. Yanga wamekuwa bora sana msimu huu. Stephen Aziz KI, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Yao Kouasi wamekuwa moto sana. Historia na rekodi kuelekea mechi hiyo huwa hazina msaada.

Takwimu za matokeo yaliyopita, ubora na udhaifu wa timu moja navyo huwa havina msaada. Mechi ya Dabi ya Kariakoo ni nzuri kuzungumza baada ya kuchezwa. Kila siku inakuja tofauti. Kila siku inakuja na matokeo ya kushangaza. Pamoja na kuwa Yanga ni bora sana msimu huu kuliko Simba, hakuna aliyedhani mechi ya mkondo wa kwanza Yanga itashinda 5-1.

Mashabiki wa Yanga wanaitaka mechi, mashabiki wa Simba wanaiogopa Aprili 20. Msimu huu kwa Simba ni kama ulimalizika siku walipofungwa 5-1 na Yanga. Tangu hapo Simba haijawahi kukaa sawa. Najua Dabi ya Kariakoo ndiyo sehemu ambapo Simba inatakiwa kumaliza msimu kwa furaha. Kimahesabu, bado Simba wanaweza kutwaa ubingwa wa ligi lakini kiuhalisia nafasi yao ni ndogo. Ili kukufua matumaini ni lazima washinde mechi na Yanga. Kwa utamaduni wa mpira wetu, Kariakoo Dabi ni kama kombe lingine. Kufungwa mechi hiyo kocha anaweza kutimuliwa au kutimka. Viongozi wanaweza kupotea. Mashabiki wanaweza kukataa tamaa kabisa. Hii ni mechi ya kurudisha heshima ya Simba.

Hii ni mechi ya kutangaza ubingwa kwa Yanga. Kila mtu anaitaka ili kutengeneza heshima mjini. Hata kama Simba hana msimu mzuri sana lakini akishinda hii mechi mashabiki watapata cha kutambia hadi msimu ujao. Hii mechi inayoweza kuleta utulivu klabuni na heshima mtaani.

Yanga baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelod Sundowns, ni kama hasira zinaelekea kwa Mnyama. Wameshaonja ushindi wa 5-1. Wanaona dalili za kwenye kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo. Wanaona dalili za kuendelea kumnyanyasa Mnyama. Hapo ndipo ugumu wa mechi hii unapokuja.

Kila mtu anaitaka hii mechi kutengeneza heshima. Kila mtu anaitaka kutimiza malengo yake.

Moja kati ya shida kubwa za Simba ni kushuka viwango kwa wachezaji wazawa. Kumekuwa na lawama nyingi kwa viongozi juu ya usajili wa wachezaji wa kimataifa, lakini nadhani shida kubwa ipo kwa wachezaji wazawa. Wakati Simba inatamba miaka ya  karibuni, Jonas Mkude, Aishi Manula, Shomary Kapombe, John Bocco, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni na Mzamiru Yassin walikuwa kwenye ubora wa hali ya juu.

Kikosi cha Simba kwa sasa mzawa mwenye mwendelezo wa ubora ni Kibu Dennis pekee. Kuelekea Kariakoo Dabi, unahitaji kuona Kapombe na Tshabalala wakiwa kwenye ubora wa juu. Yanga wako bora kutokea pembeni. Yao Kwasi na Joyce Lomalisa ni walinzi wa kisasa ambao muda wote wako juu kushambulia. Unahitaji kuwa na watu bora wenye uwezo wa kuwazuia hawa wabeki ambao timu ikiwa na mpira muda wote wanacheza kama mawinga. Pale kati Fabrice Ngoma amekuwa fundi sana wa boli, shida ipo kwa mtu atakayecheza naye.

Kama Mzamiru Yassin atakuwa kwenye kiwango kizuri atawafanya Simba kuwa bora maana wanaenda kukutana na Mudathir Yahya, Khalid Aucho na Nzengeli ambao kiukweli wamejaa nishati. Wanafanya ukuta wa Yanga kuwa imara sana kuanzia kwenye kiungo. Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha anaweza kuamua kuja na muunganiko wa Ngoma na Sadio Kanoute, shida ni moja tu Kanoute ana matumizi makubwa ya nguvu na amekuwa sio mzuri sana kutengeneza mashambulizi. Kugongana na kina Mudathir, Pacome na Aziz KI kwa dakika 90 kunaweza kuleta kadi mbili za njano.

Hii Dabi haijawahi kuwa na mwenyewe. Kabla ya mechi unaweza kuhisi kama Simba hatoboi lakini baada ya mechi usishangae Miguel Gamondi akapewa mkono wa kwaheri. Hizi ni mechi zenye hadhi ya fainali kwenye soka letu. Yanga wamekuwa bora sana lakini wakifungwa na Simba utulivu huwa unapotea. Ni mechi zinazosababisha uamuzi wa ajabu kwenye soka letu. Kuna mchezaji anaweza kufanya kosa Aprili 20, hautakuja kumuona tena akiwa na timu hiyo.

Kila mtu ana presha. Wachezaji, makocha, viongozi na mashabiki hakuna anayemuamini mwenzake. Hizi ndizo mechi ambazo makosa ya mwamuzi yanaweza kumtoa rais wa klabu madarakani. Ni shutuma juu ya shutuma. Kama kuna kitu ambacho Bodi ya Ligi wanapaswa kutusaidia ni kutupatia waamuzi bora.

Mambo ya kusema mpira ulivuka mstari au haukuvuka hatutaki kuyaona kwenye Kariakoo Dabi. Ikiwezekana ule utamaduni wa kuweka waamuzi sita kwenye mechi ungerudi. Ni muhimu kwa Azam TV kuweka kamera za kutosha hasa eneo la goli.

Ni muhimu kuwa na waamuzi wengi uwanjani ili kuondoa kelele zinazoweza kuepukika. Itapendeza kama mtu atafungwa kihalali kwa Mkapa. Itapendeza kama mechi itamalizika watu wakiwa wameridhika na uamuzi.