Mwinyi, Aggrey watemwa Stars

Muktasari:
Wachezaji hao wamechukua nafasi ya Aggrey Morris na Haji Mwinyi walioondolewa kikosini kutokana na mkanganyiko wa kutafsiri sheria.
Dar es Salaam. Beki wa Azam, Gadiel Michael na beki wa Prisons Nurdin Chona wameitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachoondoka leo kwenda Misri kuweka kambi ya siku nane.
Wachezaji hao wamechukua nafasi ya Aggrey Morris na Haji Mwinyi walioondolewa kikosini kutokana na mkanganyiko wa kutafsiri sheria.
Kocha wa Taifa Stars amesema amewaondoa wachezaji hao kwa sababu ya uelewa wa jamii.
"Nimewaondoa ili kuepuka mkanganyiko wa kutafsiri kanuni baada ya Zanzibar kupata uanachama.Wananchi wengi wanahoji kwanini wachezaji hawa wajumuishe Stars ilihali wanatoka Zanzibar," alisema Mayanga.
Wachezaji hao 21 kutoka hapa Tanzania wataungana na nahodha Mbwana Samatta na Faridi Mussa kufanya jumla ya wachezaji kuwa 23 watakaokuwa nchini Misri.
Nahodha nsaidizi, Jonas Mkude hatakuwako kwenye msafara huo kutokana na ushauri wa madaktari walioelekeza kwamba nyota huyo wa Simba apate mapumziko ya angalau siku nne.
Mkude ataungana na wenzake Juni 8, mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri.
Mchezo dhidi ya Lesotho utafanyika Juni 10, ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 nchini Cameroon.
Mbali ya Lesotho na Tanzania, mechi nyingine ya kundi hilo itawakutanisha Uganda na Cape Verde.
Kikosi cha Taifa Stars kinaundwa na makipa Aishi Manula (Azam FC), Benno Kakolanya (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Mabeki Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC), Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael (Azam). Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons).
Viungo ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na timu kwa sasa.
Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba) na Mzamiru Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba ), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting).
Wasaidizi wa Mayanga katika benchi la ufundi ni kocha msaidizi, Novatus Fulgence, kocha wa makipa Patrick Mwangata,Meneja wa timu, Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu, Daktari wa timu ni Richard Yomba na Daktari wa viungo ni Gilbert Kigadya.