Mwigulu amtaja Morrisson, Makambo bungeni
Muktasari:
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewataka mashabiki wa Yanga kuachana na suala la Bernard Morrison kwa kuwa straika Heritier Makambo anarudi Jangwani.
Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewataka mashabiki wa Yanga kuachana na suala la Bernard Morrison kwa kuwa straika Heritier Makambo anarudi Jangwani.
Mwigulu amesema hayo leo Jumanne Juni 22, 2021 wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Jana Jumatatu Gazeti la Mwanaspoti liliandika habari kuwa straika Heritier Makambo anajiandaa kurudi Jangwani baada ya kuanza mazungumzo ya siri na mabosi hao wa Yanga.
Waziri Mwigulu ambaye katika majumuisho yake ya hoja za wabunge amezungumzia amewataka Wanajangwani kutulia maana Makambu anatua.
“Niwapongeze wana Yanga ambao wamewaunga mkono Simba kwa kuwapa Morrison licha ya Wanasimba kuwa na mashabiki wenye heshima, wengine tunao humuhumu (bungeni), hawakuwahi kurudisha hata tiketi ambayo Yanga walimletea Morrison Yanga” amesema Waziri Mwigulu na kuongeza
“Yanga endeleeni na upendo huohuo, waachieni tu Morrison maana anakuja Makambo” amesema Dk Mwigulu ambaye pia ni shabiki wa Yanga.
Aipigia saluti Simba
Waziri Mwigulu amesema kuwa kutokana na ubora wa kikosi Simba, alitegemea wangefika fainali Ligi ya Mabingwa Afrika lakini kilichowakwamisha ni kujiandaa zaidi na mechi ya watani badala ya mechi ya kimataifa.
Simba ilitolewa katika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na Kaizer Chief ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3 ambapo mchezo wa kwanza war obo fainali simba ilifungwa mabao 4-0 huku mchezo wa marudiano uliopigwa katika uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, Simba ilishinda 3-0.
Waziri Mwigulu ambaye alikuwa anazungumzia masuala ya ushiriki wa klabu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa amesema kuwa kinachoangusha timu za Tanzania ni kutokuwa na mipangilio ya vipaombele.
“Spika tumeongelea sekta ya michezo, hili naongea kama mwanamichezo sio kama shabiki, kwenye michezo bado tunakosea kwenye mipangilio, vitu vyetu vingi bado vinakuja kwa dharura” amesema Mwigulu ambaye ameipongeza Simba kwa hatua iliyofikia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kwanza niipongeze Simba wamefanya makubwa sana mwaka huu, mimi nilivyokuwa naiangalia Simba ya mwaka huu ilikuwa ya kwenda kuchukua ubingwa”amesema
“Kuna mahali tumekosea na tunakosea pale ambapo hatuweki vipaombele, yani sisi kwetu mambo yako sawa tu” ameongeza
Amesema kuwa inapotokea klabu ya Tanzania inashiriki michuano ya kimataifa inapaswa michuano hiyo kupewa kipaombele na kuzitaka mamlaka za hapa nchini zinazohusika na soka kuliangalia kwa upekee suala hilo hasa kwenye ratiba za ndani.
“Kwamba mtu anaende kucheza mchezo ambao unaweza kuleta kombe kwa mara ya kwanza Tanzania, sasa mtu (Simba) anaenda kucheza mchezo mkubwa wa kwenda nusu fainali ya Kombe la Mabingwa Afrika katikati yake unaweka mechi ya watani” amesema Dk Nchemba
Dk Mwigulu ambaye ni shabiki wa Yanga amesema kuwa mchezo wa Watani wa Jadi kati ya Simba na Yanga uliharibu mipango ya maandalizi ya Simba kujiandaa Kuwakabili Kaizer Chief ya Afrika Kusini badala yake Simba iliweka nguvu nyingi kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Yanga
“Mimi nilivyoona Simba imefungwa kule Afrika ya Kusini, wao na wengine wanaaminishwa kuwa wamehujumiwa na yule Senzo na wengine wanaaminishwa kuwa wamehujumiwa na watani, kiuanamichezo kabisa tunakosa mpango” amebainisha Waziri Mwigulu nakuongeza
“Simba imeenda kucheza Afrika Kusini bila game plane, yenyewe ilijiandaa na mechi ya mtani, na mimi niwapongeze Yanga walivyoenda wakakaa dakika kadhaa wakaona Simba hawapo wakajua wanajiandaa na mchezo hawa” amesema
Amezitaka mamlaka zinazohusika na kupanga ratiba za michezo ziangalie namna ambavyo ratiba haziingiliani na mechi za kimataifa
“Spika on a serious note timu zinazoenda kwenye mashindano ya kimataifa zinaleta sifa ya Taifa, lazima bodi hizi zinazosimamia wawe wanawapa kipaombele, wangeweza kupeleka mchezo mbele kwa sababu leo hii timu zetu hata kama ni fainali ya kimataifa lakini ukiweka mechi ya mtani hapa akili zote na miundombinu yote inaelekea hapo“ amesema na kuongeza
“Simba hii iliyompiga Al Ahly ingehujumiwa na Senzo kweli? Eti ilihujumiwa na mashabiki? Hapa walenda bila game plan”