Mwendwa atua Dar kukutana na mabosi Simba

WINGA wa kimataifa Mkenya Harrison Mwendwa amewasili nchini asubuhi ya leo akitokea mapumzikoni nchini kwao baada ya Ligi ya Zambia kumalizika akicheza katika klabu ya Kabwe Warrios.

Inaelezwa Mwendwa amewasili hapa nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kimkataba na Simba iliyoonyesha nia ya kumuhitaji tangu dirisha dogo la msimu huu mwezi Januari.

Taarifa inaeleza kama Mwendwa atakubaliana na Simba katika mazungumzo hayo atasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo na kama mambo hayatakwenda vizuri atafanya maamuzi mengine kwani kuna timu zinamuhitaji hapa nchini na Afrika Kusini.

Winga huyo anayetumia mguu wa kushoto aliwahi kutamba na timu za Mathare United, Kariobangi Sharks na AFC Leopards amekuwa akiwindwa na Simba tangu kwenye dirisha dogo la usajil la msimu huu na Mwanaspoti liliwajulisha na hata dili lilipokwama tulianika sababu zake.

Taarifa inaeleza Mwendwa kwa sasa ni mchezaji huru na baada ya mkataba wake na Kabwe kumalizika, huku ikielezwa anasakwa pia na klabu za Afrika Kusini na Azam, japo Simba ikipewa nafasi kubwa ya kumnasa.

Kwa muendelezo wa taarifa huu usiache kusoma gazeti lako la Mwanaspoti kwenye toleo la kesho Jumamosi.