Simba yavuta winga, kutua Dar leo

WAKUBWA wawili wa Simba wapo Ghana kutafuta mashine mpya zitakazokuja kuongeza makali ya kikosi hicho, lakini za moto kabisa ni kwamba leo Ijumaa kuna kitu kinatua Dar es Salaam kutoka Kenya.

Ni winga matata kutoka Kenya ambaye wanakuja kumalizana kwa ajili ajili ya msimu ujao wa michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

Mkenya huyo ni Harrison Mwendwa anayetokea Kabwe Warriors ya Zambia.

Winga huyo anayetumia mguu wa kushoto aliwahi kutamba na timu za Mathare United, Kariobangi Sharks na AFC Leopards amekuwa akiwindwa na Simba tangu kwenye dirisha dogo la usajil la msimu huu na Mwanaspoti liliwajulisha na hata dili lilipokwama tulianika sababu zake.

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa, Mwendwa atawasili nchini leo akitokea kwenye mapumziko Nairobi.

Taarifa inaeleza Mwendwa kwa sasa ni mchezaji huru na baada ya mkataba wake na Kabwe kumalizika, huku ikielezwa anasakwa pia na klabu za Afrika Kusini na Azam, japo Simba ikipewa nafasi kubwa ya kumnasa.

Simba katika kuonyesha wapo siriazi na jambo hilo, wamemuita nchini na atawasili leo kukamilisha jambo lake na huenda akatambulishwa wikiendi hii.

Alipotafutwa na Mwanaspoti, Mwendwa alisema amekuwa na ofa nyingi kutoka kwenye timu mbalimbali ila kati ya hizo kuna moja yenye maslahi mazuri atakubaliana nayo baada ya kushauriana na viongozi wake.

“Maamuzi na hatma yangu ya msimu ujao si muda mrefu itafahamika kama nitarudi Zambia au kwenda mahala pengine ila wakati huu natamani kucheza karibu na nyumbani Kenya,” alisema Mwendwa, aliyezaliwa Septemba 4, 1992.

Mabosi wa Simba wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Try Again kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisisitiza watafanya usajili wa wachezaji bora ili kuongeza makali ya kikosi cha msimu ujao.

Muda wowote Simba itatangaza kupukutisha baadhi ya mastaa waliochemsha huku ikiendelea kushusha silaha mpya kwa hasira kubwa zaidi.