Mwanza kuimiliki Pamba, yaahidi kuutafuna mfupa wa Ligi Kuu

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla akizungumza katika kikao maalum cha kuikabidhi timu ya Pamba mikononi mwa halmashauri ya Jiji la Mwanza
Muktasari:
- Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza, Aaron Kagurumjuli ndiye aliyeipandisha ligi Kuu, KMC inayomilikiwa na halmashauri ya manispaa ya Kinondoni mwaka 2018 akiwa mwenyekiti wa timu hiyo na mkurugenzi wa manispaa hiyo na ameapa kufanya hivyo akiwa na Pamba.
Mwanza. NI rasmi Halmaahauri ya Jiji la Mwanza imefikia makubaliano ya kuimiliki Klabu ya Pamba ikisimamia uendeshaji, umiliki, na malipo ya wachezaji na benchi la ufundi, huku ahadi ya kwanza ikiwa ni kuipandisha daraja kwenda Ligi Kuu baada ya kukwama kwa zaidi ya miaka 20.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Julai 14, 2023 jijini hapa katika kikao maalum kilichosimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, Mkurugenzi wa Jiji, Aaron Kagurumjuli, viongozi wa Chama cha soka mkoa (MZFA), viongozi wa timu ya Pamba na wadau mbalimbali wa soka mkoani hapa.
Hivyo, klabu hiyo sasa ni mali ya halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo lengo la uamuzi huo ni kuifanya timu hiyo kujiendesha kwa ufanisi, kutatua changamoto ya fedha na kuirejesha mikononi mwa wananchi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ilipokuwa inaendeshwa na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).
Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza, Aaron Kagurumjuli amesema kuanzia sasa halmashauri hiyo itasimamia kila kitu ambapo kwa sasa wanaendelea na taratibu za kukamilisha uhamisho huo.
"Lengo kubwa ni kuhakikisha Pamba inasimama kwa miguu yake na wachezaji kuwa na uhakika wa kucheza na kuendeleza vipaji vyao, kwahiyo kuanzia leo tutasimamia kila kitu, wananchi wa Mwanza watarajie timu bora na watarajie timu yao kuingia Premier league (Ligi Kuu)," amesema Mkurugenzi huyo
Mwenyekiti wa klabu ya Pamba, Evarist Hagila amesema timu hiyo ilikuwa na uhitaji mkubwa wa fedha kujiendesha hivyo hatua hiyo imeiweka klabu hiyo katika mikono salama, huku akieleza kuwa kwa sasa hawawajibiki tena na timu hiyo kwani wanakamilisha tu taratibu za makabidhiano na kila kitu kitasimamiwa na halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiwamo madeni ya wafanyakazi.
"Timu sasa hivi iko chini ya Jiji sisi kama viongozi tunasubiri maagizo ya jiji na tunajihesabu kwamba kuanzia leo (Ijumaa) siyo viongozi wa Pamba lakini tupo kwa ajili ya kuhakikisha mchakato wa makabidhiano unakamilika," amesema
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano amesema "Sisi tumelipokea jambo hili kwa mikono miwili kwa sababu timu hiyo imekuwa ikihangaika sana kiuchumi tangu ilipoachwa na Bodi ya Pamba,"
"Utaratibu utakapokamilika basi tunaamini furaha ya ile Pamba tunayoifahamu itakuwa imekamilika, sasa mpira unarudi, hakutakuwa na kuunga unga, mpira sasa utachezwa kwa sababu mpira unahitaji uwekezaji," amesema Mwenyekiti huyo