Mwandembwa apewa Simba, Yanga Kwa Mkapa

Tuesday May 04 2021
WAAMUZI PIC
By Ramadhan Elias

KUELEKEA Mei 8 itakapopigwa mechi ya Ligi Kuu Bara itakayozikutanisha timu vigogo wa ligi hiyo Simba na Yanga, mapema leo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza waamuzi watakaosimamia mchezo huo.

Katika mechi hiyo mwamuzi namba moja amepangwa kuwa Emmanuel Mwandembwa kutokea Arusha wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Ramadhan Kayoko kutokea Dar es Salaam.

Eneo la waamuzi wa pembeni kwa maana ya washika vibendera, namba moja atakuwa Frank Komba kutokea Dar es Salaam huku namba mbili akiwa Hamdani Said kutokea Mtwara.

Katika mchezo huo uliopangwa kuchezwa Jumamosi ya wiki hii, Simba ndio watakuwa wenyeji ikiwa ni mchezo wa marudiano baada ya ule wa awali uliopigwa Novemba 7 mwaka jana Yanga wakiwa wenyeji kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Hadi sasa Simba ndio vinara wa Ligi Kuu msimu huu wakiwa na alama 61 walizozivuna kwenye mechi 25 walizocheza huku wapinzani wao Yanga, wakiwa nafasi ya pili na alama  57 baada ya kucheza mechi 27.

Advertisement