Mwanaspoti lasepa na Simba, DR Congo

Msafara wa Simba kuelekea DR Congo kuivaa AS Vita unaondoka leo saa 1.00 jioni lakini jambo la kufurahisha ni kwamba Mwanaspoti itakuwa 'live' kujulisha umma kila kinachojiri huko Kinshasa.
Jopo hilo linaloenda DR Congo, linaongozwa na vigogo watatu wa timu hiyo ambao ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi,Mshauri Mkuu wa Masuala ya kiufundi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez.
Simba itaondoka na usafiri wa Ndege ya Shirika la Ethiopia ikiwa imeambatana na mwandishi wa Mwanaspoti, Thobias Sebastian ambaye atakuwa akiripoti taarifa mbalimbali kuanzia safari yenyewe hadi mchezo baina ya Simba na AS Vita utakaochezwa kwenye Uwanja wa Martys jijini humo, Februari 13.

Kikosi cha wachezaji 27 wa Simba kwa sasa kimeshafika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na tayari kimeshafanyiwa ukaguzi na wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi pamoja na baadhi ya viongozi wa timu hiyo wanasubiria tu muda wa safari ili wakwee pipa na kuanza safari ya kwenda DR Congo.
Msafara huo unatarajiwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Ethiopia mnamo saa 4.15 usiku na baada ya hapo italazimika kusubiri na kubadilisha ndege tayari kwa safari ya kwenda Kinshasa ambayo inakadiriwa itatumia takribani saa 4.
Kikosi cha wachezaji 27 wa Simba amb acho kipo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julisu Nyerere jioni hii kikielekea DR Congo kinaundwa na makipa Aishi Manula, Ally Salim na Beno Kakolanya wakati mabeki ni Shomari Kapombe, Ibrahim Ame, Joash Onyango, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Peter Muduhwa, Kennedy Juma, Gadiel Michael na Mohamed Hussein
Viungo ni Taddeon Lwanga, Jonas Mkude, Rally Bwalya, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Hassan Dilunga, Ibrahim Ajibu, Clatous Chama na Francis Kahata wakati washambuliaji ni Bernard Morrison, Medie Kagere, Miraji Athuman, Chris Mugalu na Junior Lokosa.