Mwanasheria ataja kitakachomkuta Mwakinyo

Muktasari:
- Juzi, kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Amiri Msumi aliyetoa uamuzi wa bondia huyo kupelekewa wito wa kufika mahakamani kupitia gazeti baada ya Mwakinyo kukataa kupokea hati ya wito iliyowasilishwa kwake na msambaza nyaraka wa Mahakama.
WAKATI Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikielekeza bondia Hassan Mwakinyo kupelekewa wito wa kufika mahakamani kupitia gazeti la Mwananchi kufuatia kesi ya madai inayomkabili, wakili kiongozi wa kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza, Alloyce Komba amebainisha mambo yanayoweza kumkabili kama ataendelea kutotokea.
Juzi, kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Amiri Msumi aliyetoa uamuzi wa bondia huyo kupelekewa wito wa kufika mahakamani kupitia gazeti baada ya Mwakinyo kukataa kupokea hati ya wito iliyowasilishwa kwake na msambaza nyaraka wa Mahakama.
Akizungumza kwa muktadha wa kisheria, Komba alisema Mwakinyo hawezi kukwepa hiyo kesi na kama ikitokea hatafika mahakamani upande wa mashtaka utaomba isikilizwe upande mmoja na Mahakama haiwezi kukataa.
“Kupelekewa wito wa kufika mahakamani kupitia gazeti ni samansi mbadala. Kama Mwakinyo atakwenda mahakamani Novemba 20, 2023 ili kusikiliza kesi yake itakapotajwa tena, basi itasikilizwa pande zote mbili na kujitetea.
“La sivyo upande wa mdai ukiomba isikilizwe upande mmoja ikileta ushaidi wake (ex parte hearing) ikaamuriwa hivyo, Mwakinyo hatatafutwa tena matokeo yake ni asubiri hukumu ya upande mmoja (ex parte judgment) ambayo huwa na madhara makubwa.
“Mdai akishinda atapata decree (ya kukazia hukumu) anaweza kukamata akaunti za benki au mali zake mdaiwa,” alisema. Komba akifafanua kwamba ili kesi isikilizwe pande zote ni upande wa Mwakinyo kufika mahakamani.
Bondia huyo alifunguliwa kesi ya madai na kampuni ya PAF Promotion kuilipa Sh150 milioni ikiwa ni madhara ya jumla iliyopata baada ya kutopanda ulingoni tofauti na mkataba aliosaini wa pambano la Septemba 29. Bondia huyo awali alidai sababu za kutopigana ni promota kukiuka makubaliano.
Wakili anayewakilisha PAF Promotion, Herry Kauki alidai walipeleka wito Serikali ya mtaa, lakini Mwakinyo aligomea kupokea wito wa kufika mahakamani. Na pia walimtuma msambaza nyaraka wa Mahakama maalumu kupeleka viapo, pia aligoma kupokea, hivyo msambaza nyaraka alikula kiapo kueleza amepeleka wito lakini Mwakinyo amekataa kusaini wala kupokea.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Msumi alitoa amri upande wa mlalamikaji kutangaza wito wa Mahakama katika gazeti la Mwananchi ukimtaka Mwakinyo kufika mahakamani Novemba 20, 2023 ili kusikiliza kesi yake.
Akizungumza kisheria, Komba alisema: “Kupelekewa wito kupitia gazeti ni hatua ya mwisho. Hatua ya pili baada ya kugoma kupokea ni samansi kubandikwa kwenye nyumba yake au serikali ya mtaa, samansi mbadala ikichapishwa kwenye gazeti mdai atakwenda na ushahidi wa gazeti mahakamani na kuomba kesi isikilizwe upande mmoja.”