Mwanangu Simba

Kocha Joseph Omog
Muktasari:
Mashabiki hao wanapaza sauti mitaani huku wakijipiga kifua wakisema; ‘Waleteni hao Yanga tuwanyooshe’.
ACHANA na matokeo ya sare ya bao 1-1 iliyopata jana Jumapili dhidi ya URA ya Uganda, kikosi cha Simba chini ya Kocha Joseph Omog na Msaidizi wake, Jackson Mayanja kimetulia mwanangu.
Simba itakayoivaa Yanga katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu Oktoba Mosi, jijini Dar es Salaam kwa sasa inacheza soka la kuvutia, lenye hesabu na linaloeleweka kiasi kwamba mashabiki wao mitaani sasa wanatamba.
Mashabiki hao wanapaza sauti mitaani huku wakijipiga kifua wakisema; ‘Waleteni hao Yanga tuwanyooshe’.
Wanaamini hawawezi kupigwa tena nje ndani kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa sababu katika mechi chache ambazo timu yao imecheza, zikiwamo mbili za kimataifa zimewatia mzuka kinoma wakiamini hata ubingwa msimu huu ni wao.
WAIBANA URA
Jana Jumapili kikosi hicho kilikuwa kikicheza mchezo wa kirafiki maalum wa kumuaga nahodha wao, Mussa Hassan Mgosi na waganda nusura wawatibulie walipotangulia kupata bao, kabla ya Wekundu hao kutuliza na kurejesha bao.
URA waliandika bao dakika ya 20 kupitia kwa Nkugwa Elikanah kabla ya Jonas Mkude kusawazisha dakika 12 baadaye, huku Laudit Mavugo akiendelea kuwa gumzo kwa kiwango chake cha soka alichokionyesha akicheza kwa dakika 90.
MGOSI AAGWA
Mussa Hassan Mgosi aliagwa rasmi baada ya kustaafu kuichezea timu hiyo na kuwa meneja mpya wa Simba. Mgosi alicheza dakika sita za mwanzo za mchezo huo na kutolewa ambapo alipokelewa na mkewe pamoja na familia yake na kuzunguka uwanja mzima akiwaaga mashabiki wa timu hiyo.
Vijana hao wa Omog walionyesha kandanda tamu na kama si umakini mdogo ni wazi wangerejea kile walichoifanyia AFC Leopards walioinyuka mabao 4-0 wiki iliyopita katika tamasha la Simba Day.
Pambano hilo lilianza kwa kasi na Simba ilifika katika lango la URA katika dakika ya kwanza tu lakini hakukuwa na madhara yoyote.
URA walionekana kucheza kwa kutulia na kuwa wa kwanza kupiga shuti kwenye lango la Simba kupitia kwa straika wao Lakota Labama katika dakika ya 19 kabla ya dakika moja baadaye Elikanah kuwafungia wageni hao bao la kuongoza.
Simba ilitulia na kufanya mashambulizi kadhaa kupitia kwa Ibrahim Ajibu na Shiza Kichuya kabla ya Mkude kuisawazishia Simba katika dakika ya 32 akifunga kwa kichwa baada ya kuunganisha faulo ya Mohammed Hussein na kuibua shangwe uwanjani hapo.