Mwamnyeto: Msikonde, huku hatuachi kitu

Saturday January 15 2022
mwamnyeto pic
By Charity James

MASHABIKI wa Yanga bado wana hasira kutokana na chama lao kushindwa kutinga fainali ili kutetea wao wa Kombe la Mapinduzi, lakini nahodha wa timu hiyo, Bakar Mwamnyeto amewatuliza, akiwaambia wasikonde watapambana kubebea mataji yaliyosalia.

Yanga imesaliwa na mataji mawili tu ya kuyapambania msimu huu, Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC, yote yakishikiliwa na Simba ambayo usiku wa jana ilikuwa ikimalizana na Azam katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi 2022, baada ya Yanga kulitema taji mapema.

Mwamnyeto alisema ni kweli matokeo ya kushindwa kutetea ubingwa wao, yamewaumiza na sio mashabiki tu bali hata wao wachezaji na benchi zima la ufundi, lakini hawajakata tamaa kwani wanajipanga kuhakikisha wanabeba mataji yaliyobaki.

“Tuna Ligi Kuu na Kombe la FA (ASFC) hatuna sababu ya kukata tamaa, tulipambana kwa nia ya kutwaa mataji yote, lakini moja limeponyoka, sasa tutapigania mataji yaliyobaki, mashabiki wetu wasikatie tamaa. tumekosea hatuwezi kurudia makosa,” alisema Mwamnyeto na kuongeza;

“Tumesahau yaliyopita akili zetu zinahamia Ligi Kuu tunatarajia kukutana na Coastal Union ni mchezo mgumu kwetu hatuwezi kutoka kupoteza tukaendeleza tulipoishia tutapambana kupata matokeo.”

Naye straika wa timu hiyo, Heritier Makambo alisema matokeo ya Azam ilikuwa sapraizi kwao kwani mipango yao ilikuwa ni kutetea taji.

Advertisement

“Kila mmoja wetu hakuamini kilichotokea tulijiamini na tulitarajia matokeo mazuri lakini haikuwa hivyo tuliyapokea japo kwa maumivu tunajipanga kwa mataji mengine,” alisema Makambo ambaye aliuzungumzia mashindano hayo kwa ujumla, alidai amepata muda mwingi wa kucheza na umemrudisha kwenye hali nzuri ya ushindani wakati ligi ikirejea tena.

Yanga itacheza mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara keshokutwa Jumapili ugenini dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, ambako Wanajangwani walipasuka 2-1 na kuvurugiwa rekodi yao ya kupototeza katika mechi 32 mfululizo za Ligi Kuu. Bara,

Advertisement