Mwakinyo, Class wavuliwa ubingwa WBF

HABARI mbaya kwa mabondia bora nchini, Hassan Mwakinyo na Ibrahim Class ni kuvuliwa kwa mataji ya ubingwa wa WBF. Mabondia hao wanaokamata nafasi ya kwanza na ya pili kwa ubora kwenye kila uzani nchini wamevuliwa mikanda hiyo ya ubingwa wa Shirikisho la ngumi za kulipwa la dunia la WBF.
Taarifa iliyotolewa na WBF ilieleza mabondia hao si mabingwa tena wa Shirikisho hilo lenye makao makuu yake nchini Afrika Kusini. Taarifa hiyo ilisema mikanda ya WBF kwenye uzani wa super welter na super feather ambayo walikuwa wakiishikilia Mwakinyo na Class iko wazi. “WBF tumeumizwa na hiki kilichotokea, lakini kwa mujibu wa kanuni, hawa si mabingwa wetu tena baada ya kushindwa kutetea ubingwa kwao kwa wakati,” ilisema taarifa hiyo. Class bondia namba moja kwenye uzani wa super feather nchini alitwaa taji hilo Januari 29, 2021 alipomchapa Denis Mwale kwa pointi na kutawazwa kuwa bingwa mpya wa mabara wa WBF kwenye uzani wa light.
Mwakinyo yeye alitwaa taji hilo Agosti 14, 2020 alipomchapa Bebe Rico Tshibangu kwenye uzani wa super welter na kuutetea Novemba 12 mwaka huo alipomchapa Jose Carlos Paz kwa TKO, mapambano yote yalipigwa Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), Yahya Poli alisema wana taarifa za Mwakinyo kuzuliwa taji hilo na bingwa ambalo sasa linashikiliwa na Victor Lonescu wa Romania.
“Kwa Class hatujapata taarifa hizo, ingawa kila Chama cha ngumi kina sheria zake na uwa wanatoa muda kwa mabingwa wao kutetea mataji hayo vinginevyo wanavuliwa,” alisema Poli.