Mwaikimba awatungua wapinzani wa Yanga

Muktasari:
Mshambuliaji huyo alitamba akiwa Yanga, Azam na timu ya taifa Taifa Stars
Kyela. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Gaudence Mwaikimba ameiongoza timu yake ya Boma Fc kuichapa Ihefu Fc kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili (SDL), uliochezwa kwenye Uwanja wa John Mwakangale wilayani Kyela.
Mwaikimba alifunga bao hilo pekee kwa Boma kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 65, baada ya mchezaji wa Ihefu kuunawa mpira eneo la hatari.
Ushindi huo unaifanya Boma kufikisha pointi 14 ikiwa nafasi ya pili katika Kundi C baada ya kucheza mechi saba na kubakiwa na mechi tatu mkononi.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Kocha Mkuu wa Boma, Oscar Koroso alisema ni jambo la kheri kuona timu yake inajiongezea pointi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kupanda daraja.
‘’Tumuombee tu mabaya Green Warrious apoteze mechi zake zilizobaki ili sisi tukishinda hizi tatu tutakuwa na nafasi kubwa ya kupanda daraja,’’ alisema Koroso.
Kocha Koroso alisema ligi imefika sehemu ngumu kutokana na kuwa mwishoni na kwamba kila timu inajitahidi kuhakikisha haipotezi mechi hizi za lala salama.
Kwa upande wake kocha wa Ihefu Fc Michael Kasekenya alisema ingawa mpira una matokeo matatu lakini kupoteza mechi hizi za lala salama ni pengo lisiloweza kuzibika.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Ihefu fc umemtimua aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Salhina Mjengwa na mikoba yake kwa sasa amepewa kocha Kasekenya aliyekiongoza kikosi hicho juzi kwa mara ya kwanza.
Ihefu inajiandaa na mechi ya kombe la FA dhidi ya Yanga itakayochezwa mwishoni mwa mwezi huu.