Mwadui yaivunja rekodi ya Simba kibabe Ligi Kuu Tanzania Bara

Muktasari:
Huu ni ushindi wa pili wa Mwadui tangu ilipopanda ligi msimu wa 2015-16, katika michezo tisa wamefungwa mitano na kutoka sare michezo miwili.
Shinyanga. Mwadui imekuwa timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu baada ya kuichapa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Bao pekee la Mwadui limefungwa na Gerard Mdamu katika dakika 33, akiunganisha kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto Khalfan Mbaruku.
Ushindi huo wa Mwadui unatibua rekodi ya Simba ya kutokufungwa katika michezo sita iliyopita ya Ligi Kuu.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems atajilaumu mwenyewe kwa uamuzi wake wa kumwazisha mshambuliaji mmoja Meddie Kagere huku akijaza viungo wengi ambao walishindwa kuonyesha ubora wao.
Mwadui iliyokuwa ikicheza soka la kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza tofauti na Simba ambao walikuwa wakishambulia mara kwa mara.
Washambuliaji wa Mwadui, Nassoro Kapalata, Ludovic Venance na Mdamu wangekuwa makini wangeweza kupata mabao mengi kutokana na mapungufu ya safu ya ulinzi wa Simba.

Simba licha ya kufanya mabadiliko matatu ya kuingia Ibrahim Ajibu, Dilunga na Miraji Athumani walioingia kuchukua nafasi za Sharafeldin Shiboub, Francis Kahata na Cletous Chama walishindwa kusawazisha.
Huu ni ushindi wa pili wa Mwadui tangu ilipopanda ligi msimu wa 2015-16, katika michezo tisa wamefungwa mitano na kutoka sare michezo miwili.
Akizungumzia mchezo huo beki wa Simba, Erasto Nyoni alisema walishindwa kutumia nafasi ambazo walipata ila wenzao walipata moja ambayo wameitumia.

"Mpira ndio ulivyo tumepoteza mechi ya leo nadhani benchi la ufundi limeiona hilo na litakwenda kulifanyia kazi kwa ajili ya mchezo ujao," alisema Nyoni.
Nahodha wa Mwadui, Joramu Mgeveke alisema wamefuata maagizo ya kocha wao ndiyo siri ya mafanikio yao.
"Tulikuja kufuata pointi tatu na hata kama tukishindwa tupate sare ndio maana tumefanikisha hili la kupata pointi tatu dhidi ya Simba," alisema Mgeveke.

Katika kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kucheza soka la umaridadi huku wote wakicheza kwa kutumia nguvu pamoja na spidi katika kupeleka mpira mbele.
Dakika 9 Hassan Kapalata alipewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi kiungo Gerson Fraga katika eneo la katikati baada ya kwenda kumkwatua mguuni.
Dakika 26 Simba ilitaka kuipata bao kupitia kwa Mzamirun Yassin baada ya kiungo Clatous Chama kuwatoka mabeki wa Mwadui na kupiga pasi kwa Mzamiru Yassin aliyekunjuka shuti na kutoka nje kidogo ya goli.
Mwadui walikuwa wazuri katika eneo la katikati lililokuwa linachezwa na Mussa Nampaka ‘Chibwabwa’ pamoja na Raphael Obina na kuwafanya viungo wa Simba, Mzamiru Yassin na Clatous Chama kuhaha katika eneo hilo.

Uwezo wa viungo wa Mwadui kucheza katika uwanja wa Ccm Kambarage, ulionekana kuwa tofauti na kwa upande wa Simba ambao walikuwa wanashindwa kuumiliki mpirab ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Dakika 33 Mwadui walipata goli kupitia kwa Gerald Mathias, akionganisha kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto Khalfan Mbaruku ambaye alichungulia na kupiga mpira mrefu uliowavuka mabeki wa Simba.
Mwadui walionyesha kutulia na kufanya mashambulizi yao kwa kupitia mabeki wao wa pembeni kwa Khalfan Mbaruku na Rogers Gabriel ambao walikuwa makini katika kupiga mipira ya krosi.
Dakika 42 Mwadui walitaka kupata goli kupitia kwa Gerald Mathias ambaye alipokea kutioka kwa Khalfan Mbaruku na kutuliza na kupiga shuti lililoguswa na Gadiel Michael na kuwa kona isiyokuwa na faida.
Mshambuliahi Gerald Mathias alikuwa mwiba katika safu ya ulinzi ya Simba baada ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza mara kwa mara langoni mwa Simba.
Kagera Sugar, Mtibwa Sugar zagawa dozi
Kagera Sugar imeendeleza rekodi mbaya ya Namungo ya kufungwa ugenini baada ya kuichapa kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Kagare Sugar inayofundishwa na kocha Mecky Maxime, wamefikisha pointi 16 katika michezo minane.

Bao la Santos Mazengo lilitosha kuipa Ruvu Shooting ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Mabatini.
Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani imeshinda mechi yake ya kwanza baada ya kuchapa Coastal Union kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Lipuli ya Iringa iliifunga Polisi Tanzania kwa mabao 2-1 huku Singida United ikipokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa JKT Tanzania.