Mukoko: Yanga sasa hakuna kuremba

KIUNGO wa Yanga,Mukoko Tonombe amerejea nchini juzi usiku akitokea katika majukumu ya timu ya Taifa ya DR Congo na kusema licha ya kwamba wakati mwingine matokeo ya mpira huwa ya kikatili lakini ; “Hakuna kuremba kuanzia sasa kwenye ligi.”

Mukoko amesisitiza kwamba; “Tuna uzoefu wa matokeo ya nyuma na huku tunakokwenda panajulikana.Malengo yetu ni kutwaa ubingwa,lakini naamini hatuwezi kushindwa kirahisi kama kila mchezaji atajitoa kwa nafasi yake kuipambania timu.”

Licha ya kuiongoza DR Congo kuichapa Gambia bao 1-0 lakini walishindwa kufuzu katika Fainali za Afrika baada ya kushika nafasi ya tatu katika kundi D wakiwa na pointi tisa huku wakiziacha Gambia na Gabon zikifuzu.

Mukoko sasa amerejea kuisadia timu yake kwenye mechi za Ligi Kuu ambayo licha ya kwamba Yanga inaongoza ikiwa na pointi 50 lakini inafukuziwa kwa kasi na watani zao wa jadi Simba wenye pointi 46 lakini wakiwa na michezo mitatu mkononi.

Mukoko alisema mzunguko wa pili wa ligi ni mgumu kwani umegawanyika katika sehemu mbili, timu zinazopambania ubingwa na zile zinaopambana kutoshuka daraja.

“Hakuna ambaye hapendi ushindi licha ya kwamba wakati mwingine vile unavyotarajia inakuwa tofauti.

“Kwenye ligi kila timu inajiandaa, kuna zinazotaka ubingwa na zile zinapambana kuepuka kushuka daraja hivyo zote zinatafuta matokeo mazuri.Muhimu ni kila mchezaji katika kikosi chetu kuzidisha juhudi ili kuhakikisha tunatimiza malengo yake ya kutwaa ubingwa msimu huu,”alisema

“Nashukuru Yanga kwa kunipa heshima ya kuonyesha uwezo hapa,sasa nimerudi nataka kufanya kazi zaidi ili niweze kupata nafasi zaidi ya timu ya taifa,” alisema Mukoko ambaye leo ataripoti kambini.
“Nataka kucheza kwa kiwango kikubwa zaidi ya kile nilichofanya tangu nimefika hapa Tanzania najua nikifanya hivyo ndio nitakapoitwa tena timu ya taifa.”