Mukoko ni zaidi ya injini, Kagera ni wao wenyewe tu

Muktasari:
MABADILIKO ya kikosi ambayo yalifanyika kwa vinara wa Ligi Kuu Bara Yanga, yaliwapa nafasi Kagera Sugar kufunga mabao matatu katika kipindi cha kwanza, ingawa ilishindwa kuyalinda kwa kusawazishwa.
MABADILIKO ya kikosi ambayo yalifanyika kwa vinara wa Ligi Kuu Bara Yanga, yaliwapa nafasi Kagera Sugar kufunga mabao matatu katika kipindi cha kwanza, ingawa ilishindwa kuyalinda kwa kusawazishwa.
Kagera ilianzisha mashambulizi katika eneo la kiungo ambalo Yanga lilikuwa limepwaya hasa kwa kukosekana, Mukoko Tonombe aliyeanzishwa benchi na Kocha Cedric Kaze na kufanya Kagera watawale eneo la kiungo lililokuwa limepewa Zawadi Mauya.
Mauya alionekana wazi kushindwa kuhimili vishindo vya viungo wa Kagera na kusababisha Lamine Moro na Bakar Mwamnyeto kuonekana kupwaya kwa kushindwa kudhibiti kasi ya washambuliaji wa wageni ambao kama wangekuwa makini jana walikuwa wakiandika histori mpya dhidi ya Yanga.

Hata hivyo mabadiliko ya kumtoa Mauya na muingiza mwenye nafasi yake Mukoko iliituliza Yanga na kuifanya icheze kwa makini na kuwanyima fursa wapinzani wao kuwakimbiza kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza na kufanikiwa kusawazisha bao la tatu likifungwa na kiungo huyo kutoka DR Congo.
Katika kipindi cha kwanza Mauya akicheza sambamba na Lamine na Mwamnyeto eneo hilo la ulinzi lilikosa maelewano na kufanya makosa mengi kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ambayo walipokea kutoka kwa Peter Mwalyanzi, Hassan Mwaterema, Yusuph Mhilu na David Luhende.
Kagera nao baada ya kuona kuwa wana uwezo wa kupata mabao mbele ya Yanga walipoteza nidhamu ya kiulinzi ambayo wapinzani wao walikuwa wakitumia kusawazisha kila bao ambao walikuwa wakifunga kati ya hayo matatu.
Pengine Kagera wangekuwa imara katika eneo la ulinzi wangeweza kufanikiwa kuondoka na ushindi kwani washambuliaji wao walikuwa wakifunga, lakini walijisahau na Mukoko aliyeingia sambamba na Ditram Nchimbi na baadaye Haruna Niyonzima waliwazima na kulazimishwa sare hiyo ya 3-3.