Mugalu atuma salamu Yanga
WAKATI pambano la watani wa jadi likikaribia, straika wa Simba, Chris Mugalu amesema mabao yake mawili aliyofunga juzi dhidi ya USGN na kuiwezesha timu yake kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika yamekuja wakati mwafaka na yatamrejeshea kujiamini, jambo litakalowavuruga wapinzani.
Tangu msimu huu umeanza, huku Ligi Kuu Bara ikifikia raundi ya 19, Mugalu hajafunga bao hata moja kwenye ligi, licha ya kumaliza msimu uliopita akiwa na mabao 15 na kushika nafasi ya pili nyuma ya mshindi wa tuzo ya kiatu cha ufungaji bora, John Bocco, aliyefunga mabao 16.
Lakini juzi akiwa katika ubora wake, Mugalu alianzishwa isivyotarajiwa, hasa kutokana na mechi za siku za hivi karibuni kocha Pablo Franco kupendelea kumuanzisha Meddie Kagere, na Mcongomani huyo akafanya yake kwa kutupia mabao mawili katika ushindi wa 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mugalu aliyefunga mabao mawili kwenye mechi hiyo alisema hakuna mchezaji asiyepitia vipindi vigumu.
“Binafsi naamini nimeweza kuyafanya yote katika mchezo huo kama malengo yangu yalivyo tulishinda, nilihusika kwenye pasi za mwisho ingawa hatukutumia na niliifungia timu yangu mabao mawili muhimu,” alisema Mugalu na kuongeza;
“Naamini kwenye uwezo wangu, naweza kufunga mabao mengi zaidi ya niliyonayo sasa ila kikubwa naamini wakati huo ni sasa.”