Mtoto wa Eto'o aitwa timu ya Taifa Cameroon

Muktasari:
Eto'o anawatoto watano, ukimuondoa Etienne ambaye amefuata nyazo zake, wengini ni wa kike, ambao ni Maelle,Annie, Lynn na Siena.
MTOTO wa mwanasoka wa zamani wa Cameroon, Samuel Eto'o, Etienne amechaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa chini ya miaka 17 kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia U17 nchini Brazil.
Kinda huyo, ambaye ni nahodha wa timu ya Mallorca U-17, alisema anataka kuonyesha makali yake kwenye mashindano hayo na kuisaidia Cameroon kwa kuifungia mabao.
“Pamoja na kuwa baba yangu ni namba tisa bora, sipo hapa kuonyesha utofauti. Sina cha ziada," alisema mtoto huyo wa Eto'o kupitia kipande cha video ambacho kiliachiwa na Shirikisho la Soka nchini humo.
“Nimekuja kulisaidia Taifa langu kwa kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi," aliongeza.
Baba wa kinda huyo, Samuel, anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Cameroon akiwa na mabao 56 kwenye michezo 118 ya ushindani.
Timu ya taifa ya vijana ya Cameroon, itatupa karata yao ya kwanza kwenye fainali za kombe la dunia dhidi ya Argentina, Spain na Tajikistan katika michezo ya kundi E.