Eto’o astaafu soka rasmi, nyota Ulaya wamlilia

Muktasari:

Eto’o kupitia mitandao yake ya kijamii juzi alitangaza rasmi kuachana na maisha ya soka ndani ya uwanja, baada ya nyota yake kung’ara kwa miaka 22 akianzia mwaka 1997 katika Klabu ya Real Madrid ambayo ilitangaza jina lake vema.

Madrid, Hispania. MAMBO hufika mwisho. Samuel Eto’o Fills amejitahidi kuvuta siku za kuendelea kuwa uwanjani lakini sasa amenyoosha mikono. Amesema inatosha. Ametangaza kustaafu soka rasmi baada ya kucheza miaka 22 ya mafanikio.
Mastaa wa zamani, nahodha wake wa zamani katika Klabu ya Barcelona, Carles Puyol, nahodha wa sasa wa Barcelona, Lionel Messi, na mmoja kati ya mastaa wakubwa wa zamani wa soka la Afrika, Didier Drogba wote wamemtakia mapumziko mema.
Eto’o kupitia mitandao yake ya kijamii juzi alitangaza rasmi kuachana na maisha ya soka ndani ya uwanja, baada ya nyota yake kung’ara kwa miaka 22 akianzia mwaka 1997 katika Klabu ya Real Madrid ambayo ilitangaza jina lake vema. Staa huyo wa zamani wa Cameroon, 38, sasa amecheza katika miongoni mwa ligi kubwa tatu za Ulaya Hispania, Italia na England kabla ya kuzurura kwenda kwingineko ambako alicheza wakati uwezo wake ukiwa umeanza kupungua.
Akiwa Hispania Eto’o alicheza Real Madrid, Leganes, Mallorca, Espanyol na Barcelona kabla ya kusafiri kwenda Italia ambako alicheza Inter Milan na Sampdoria wakati England Eto’o alicheza katika Klabu za Chelsea na Everton.
Baadaye alitimkia Russia ambako alicheza Anzhi Makhachkala kisha akatua Uturuki kukipiga Antalyaspor na Konyaspor kabla ya kwenda Qatar katika Klabu ya Qatar SC ambako amemalizia maisha yake ya soka msimu uliopita akifunga mabao sita katika mechi 17.
Katika ngazi ya klabu, Eto’o ametwaa mataji yote ya soka ikiwemo kutwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na matatu ya La Liga. Lakini mara nne amefanikiwa kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika.
Wakati mastaa wengi wakimpongeza Eto’o kwa mafanikio yake ya ndani ya uwanja, staa wa Barcelona, Lionel Messi ambaye alicheza na Eto’o klabuni hapo alimtania kwamba alidhani Eto’o angeendelea kucheza soka hadi miaka 40.
“Umeamua kuacha Samu? Nilidhani ungecheza mpaka miaka 40 hivi. Bahati njema kwa kila unachotaka kufanya duniani, genius,” aliandika Messi katika ukurasa wake wa Instagramu ambao una mashabiki 130 milioni.
Naye Drogba aliandika katika ukurasa wake wa Instagram akisema: “Hongera kwa maisha mazuri ya soka Samuel Eto’o na bado kuna mwendelezo wa changamoto mpya zinazokusubiri. Afrika inajivunia kuwa na mmoja kati ya mabalozi bora kupitia wewe.”
Nahodha wake wa zamani Barcelona, Puyol naye aliandika katika ukurasa wake wa Instagram akisema: “Asante sana kwa yote kaka. Imekuwa furaha kubwa kucheza timu moja na wewe. Nakutakia bahati njema katika ukurasa wako mpya.”
Naye staa mwingine wa zamani wa Barcelona, Deco ambaye alikuwa nyota wa kimataifa wa Ureno na alitengeneza utatu mtakatifu katika kikosi cha Wakatalunya hao sambamba na nyota wa zamani wa Brazil, Ronaldinho naye alimtakia kila la kheri Eto’o huku akiandika maneno ya busara katika ukurasa wake wa Instagram.
“Mpira utakukumbuka sana kaka. Lakini, najua una mambo mengi ya kuchangia. Mpira unakuhitaji sana rafiki yangu. Ulikuwa mtu mkubwa kama mchezaji na nina uhakika utafanya kila kitu ambacho kitakuja mbele yako. Bahati njema katika hatua hii mpya ya maisha kaka,” aliandika Deco.
Eto’o anaachana na soka huku akiwa ni mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha timu ya Taifa ya Cameroon akiwa na mabao 56 katika mechi 118.
Alijiunga na Real Madrid akiwa na miaka 16 tu, lakini akaishia kucheza mechi tatu kabla ya kupelekwa kwa mkopo katika Klabu za Leganes, Espanyol na Mallorca.
Baada ya kuhamia jumla Mallorca mwaka 2000 alifunga mabao 54 katika mechi 133 na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo. Kiwango chake hicho kilisababisha Barcelona imchukue mwaka 2004 ambapo alitwaa mataji matatu ya La Liga na kuisaidia klabu hiyo ya Catalunya kutwaa mataji mawili ya Ulaya mwaka 2006 na 2009.
Mwaka 2006, Eto’o alikuwa mchezaji wa kwanza na pekee wa Kiafrika kutwaa Kiatu cha Mfungaji Bora wa La Liga wakati alipofunga mabao 26 katika mechi 34. Kwa ujumla katika kipindi chake Nou Camp alifunga mabao 108 katika mechi 144.
Aliondoka Barcelona mwaka 2009 kwenda Inter Milan ya Italia kwa uhamisho wa kubadilishana na staa wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic aliyekwenda Barcelona na akiwa na Inter alitwaa taji lake la tatu la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya pamoja na taji la Serie A na pia Klabu Bingwa ya Dunia.