Mtibwa yajipanga Ligi Kuu, yaanza na mkali wa mabao

Muktasari:
- Timu hiyo ambayo imerejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka daraja msimu uliopita, inajivunia rekodi ya kumaliza Championship ikiwa kinara kwa pointi 71.
MTIBWA Sugar imesema imebaini baadhi ya timu zinamnyatia staa wake, Raizin Hafidh hivyo imemuwahi mapema kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu huku ikidokeza mwelekeo mpya wa timu hiyo.
Timu hiyo ambayo imerejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka daraja msimu uliopita, inajivunia rekodi ya kumaliza Championship ikiwa kinara kwa pointi 71.
Pamoja na mafanikio hayo, licha ya wachezaji wote kuwa katika ubora, lakini Hafidh alionekana kuwa mtamu zaidi akifunga jumla ya mabao 23 ya mechi zote na kuihakikishia timu hiyo kupanda daraja na kufika robo fainali ya shirikisho.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Awadh Juma ‘Maniche’ alisema tayari wamekabidhi ripoti kwa uongozi kufanyia kazi mahitaji kwa ajili ya msimu ujao haswa kuboresha maeneo kadhaa ndani ya uwanja.
Maniche, alisema ripoti hiyo imewataja baadhi ya nyota walioonyesha uwezo akiwamo Hafidh, ambaye wamepata taarifa kuwindwa na timu nyingine ili kuanza naye msimu wa 2025/26.
“Raizin tuna mipango naye msimu wa 2025/26 na si huyo tu wapo wengine ambao ripoti imewataja, japo wote walifanya vizuri ila lazima tufanye maboresho kuongeza nguvu. Sehemu kama beki, kiungo na ushambuliaji tunahitaji watu wa kazi na wenye uzoefu, tunaenda kucheza Ligi Kuu ambayo kwa sasa imebadilika mambo mengi haihitaji wepesi,” alisema kocha huyo.
Maniche alisema hatua ya kushuka daraja imewapa fundisho, ambapo watajitahidi kuweka maandalizi mazuri na ya mapema kuhakikisha wasirudie yaliyowakuta na kutochezea nafasi za play off.

“Presha iliyotukuta misimu ya nyuma na kushuka daraja, hatutaki ijirudie, tunaamini uongozi nao utafanya mipango yake kuona Mtibwa inalinda heshima yake,” alisema kocha huyo.