Mtibwa Sugar yajipanga kumrejesha Kawemba

Muktasari:
- Chanzo cha taarifa hiyo kutoka ndani ya Mtibwa, kinasema jambo hilo linafanyika chini ya uongozi wa serikali ya mkoa wa Morogoro, ili kuhakikisha msimu ujao wa 2025-26 wanacheza kwa ushindani na siyo kujikwamua kushuka daraja. Kawemba alishawahi kuwa Mtendaji wa klabu hiyo miaka mitatu iliyopita.
BAADA ya Mtibwa Sugar kurejea Ligi Kuu Bara, mabingwa hao wa zamani wako katika mazungumzo ya kumhitaji Saad Kawemba ashike nafasi ya Mtendaji Mkuu wa klabu ikiamini uzoefu wake utakuwa msaada katika maeneo mbalimbali.
Chanzo cha taarifa hiyo kutoka ndani ya Mtibwa, kinasema jambo hilo linafanyika chini ya uongozi wa serikali ya mkoa wa Morogoro, ili kuhakikisha msimu ujao wa 2025-26 wanacheza kwa ushindani na siyo kujikwamua kushuka daraja. Kawemba alishawahi kuwa Mtendaji wa klabu hiyo miaka mitatu iliyopita.
“Tunahitaji Mtibwa imara kuanzia kwa wachezaji tutakaowasajili, benchi la ufundi na viongozi wanaoujua mpira wa miguu, ndiyo maana tunasaidiwa na uongozi wa serikali ya mkoa wa Morogoro ili kuwaleta Jamal Bayser aliyechukua ubingwa wa Ligi na timu hiyo misimu miwili mfululizo mwaka 1999 na 2000 na Kawemba ambaye amekuwa katika uongozi kwa klabu mbalimbali nchini,” kilisema chanzo hicho.
Kawemba pia amewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Azam na Mkurugenzi wa Mashindano Yanga, jambo ambalo viongozi wa Mtibwa wanaona litawasaidia kurejea katika makali yao.
“Kila kitu kinafanywa kwa utulivu na umakini wa hali ya juu, hadi sasa kuna CV za makocha, lakini bado hatujafanya uamuzi, tunaendelea kuangalia zaidi mtu atakayeisaidia timu kufanya makubwa,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru ili atoe ufafanuzi juu ya taarifa hiyo, alisema kwa kifupi: “Kwa sasa siwezi kulizungumzia hilo, ninachoweza kukwambia kwa sasa Mtibwa inajipanga, Watanzania watajionea kwa macho ushindani wa timu yetu kwa msimu ujao.”
Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita sambamba na Geita Gold, imerejea Ligi Kuu baada ya kuibuka kinara wa Ligi ya Championship na kubeba ubingwa, ikiwa sambamba Mbeya City ambayo ilishuka misimu miwili iliyopita.