Mtemi, Nkwabi wataka ubosi Simba

Muktasari:

  • Tofauti na chaguzi nyingine za nyuma za Simba na hata klabu nyingine majina ya wagombea wanaochukua na kurudisha fomu kufahamika kwa uwazi, Kamati ya Uchaguzi wa sasa imekuwa ikifanya mambo kwa usiri kiasi cha kuzua maswali.

WAKATI mabosi wanaosimamia Uchaguzi Mkuu wa Simba wakiendesha zoezi hilo kwa usiri mkubwa kama uchaguzi huo unafanyikia chumbani, kwa kuficha majina ya wagombea imebainika baadhi ya vigogo waliopo madarakani wamejitosa kimtindo.

Tofauti na chaguzi nyingine za nyuma za Simba na hata klabu nyingine majina ya wagombea wanaochukua na kurudisha fomu kufahamika kwa uwazi, Kamati ya Uchaguzi wa sasa imekuwa ikifanya mambo kwa usiri kiasi cha kuzua maswali.

Wanahabari waliokuwa wakiufuatilia tangu zoezi hilo lilipotangazwa walikuwa wakipewa idadi tu ya waliojitokeza bila majina kwa madai wangetajwa mwishoni, huku wapiga picha wakizuiwa kupiga picha ama kuwahoji wagombea husika.

Hata hivyo, nusanusa za Mwanaspoti limebaini kuwa, katika nafasi ya Uenyekiti walijitokeza wagombea wawili tu, Swedi Nkwabi na Mtemi Ramadhani nyota wa zamani wa klabu hiyo na timu ya taifa, Taifa Stars.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ naye ametajwa kuchukuliwa fomu za kuwania Uenyekiti, lakini alipoulizwa na Mwanaspoti alisema alishasema mapema hatagombea nafasi yoyote.

“Narudia tena sijachukua fomu na kama kuna mtu aliyemchukulia basi, mimi sijui chochote na wala hata hiyo fomu zijaiona kwani sina taarifa na bado narudia sitaki kugombea ili kuwapa nafasi wengine waiongoze Simba,” alisema Try Again.

Mbali na wagombea wa nafasi ya Uenyekiti, Mwanaspoti limedokezwa waliojitosa kwenye nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ndipo kuna orodha ndefu ya baadhi ya viongozi wa sasa na wa zamani wa klabu hiyo akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda na aliyekuwa Meneja wa timu ya Vijana iliyowaibua kina Jonas Mkude na wenzake, Patrick Rweyeimamu.

Wengine ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya sasa ya Simba, Kaimu Makamu wa Rais, Idd Kajuna, Said Tulliy, Jasmeen Badou na Ally Suru, pia wamo Asha Baraka, Mkurugenzi wa African Stars ‘Twanga Pepeta’, Hamis Ramadhani Mkomwa, Abdallah Migomba na Afred Eliya.

Katibu Mkuu wa Simba, Dk Arnold Kashembe aliyekuwepo hadi jioni zoezi lilipofungwa, alikataa kabisa kutaja majina ya waliojitokeza kwenye uchaguzi huo kwa madai mwenye jukumu hilo ni watu wa Kamati ya Uchaguzi.

“Naomba mtafute Mwenyekiti wa kamati, (Boniface Lyamwile) ndiye anayeweza kusema lolote, lakini kwangu ni vigumu, tafadhali,” alisema Dk Kashembe.

Naye Lyamwile alipotafutwa alisema alikuwa akielekea kwenye kikao cha kamati yao kilichokuwa kikifanyika Hoteli ya Serena na kutaka atafutwe baada ya saa moja ili kutaja majina ya waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo.

“Nitafute baada ya saa 1 kwani ndio kwanza tunataka kuingia kikaoni kujadili ndipo tutatangaza majina,” alisema Mwenyekiti huyo licha kubembelezwa hata kutaja idadi tu ya wagombea.