Mtango azishindwa anga za Mwakinyo

Muktasari:

  • Phiri bondia wa nyota moja na nusu anayekamata nafasi ya 243 kati ya 1732 duniani na namba tatu kati ya mabondia 10 nchini mwake kwenye uzani wa light amewahi kuwa bingwa wa WBF Afrika alipomchapa Mtanzania, Yonas Segu, Aprili mwaka jana.

Matokeo ya sare yamemkosesha ubingwa wa Afrika wa ABU, bondia namba moja nchini kwenye uzani wa super light, Salim 'Mtango' Jengo.

Bondia huyo wa nyota mbili anayekamata nafasi ya 166 kati ya mabondia 1698 duniani na namba moja kati ya mabondia 46 nchini kwenye uzani wake ameambulia sare usiku wa kuamkia leo dhidi ya Hannock Phiri wa Malawi.

Katika pambano hilo la raundi 12, si Mtango wa Phiri aliyetwaa mkanda wa ubingwa wa ABU ambao kwa sasa nchini,  Hassan Mwakinyo ndiyo bingwa wake kwenye uzani wa super welter.

Kama Mtango angeshinda jana, angeingia kwenye orodha ya mabondia mabingwa wa ABU, kwenye uzani wa super light,  taji ambalo uenda kwa baadae lingempa tiketi ya kuwania moja ya mataji makubwa duniani la WBC.

Katika pambano hilo lilolochezwa kwa mtindo wa piga nikupige kwenye ukumbi wa Millenium Tower,  Dar es Salaam, majaji walilazimika kutoa sare baada ya raundi 12 kumalizika huku Phiri akidai ameshinda, isipokuwa majaji wameamua kutoa sare.

Hata hivyo Mtango bondia anayetokea kwenye kambi ya Mwakinyo jijini Tanga alikubaliana na matokeo ya majaji akisisitiza kuwa wao ndio wenye uamuzi wa mwisho.

"Lengo langu lilikuwa ni ubingwa, lakini matokeo ndiyo hivyo nimepata droo, ndoto yangu ya ubingwa haijatimia, ila najipanga upya," amesema bondia huyo aliyekuwa akifanya sparing na Ibrahim Class.

Mtango ambaye kabla ya pambano la jana alitoka kuchapwa kwa TKO  na Shohjahon Ergashev Juni 11 mwaka huu, amewahi kuwa bingwa wa dunia wa UBO kwenye uzani wa light alipomchapa Eduardo Mancito.