Msuva Mtanzania wa kwanza kupiga bao mbele VAR Afrika

Muktasari:

Kiujumla mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kukumbana na VAR ni nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akiwa na klabu yake ya KRC Genk katika mashindano mbalimbali ya ushindani barani Ulaya.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Difaa El Jadida, Saimon Msuva ameweka rekodi ya kuwa mtanzania wa kwanza kufunga bao katika ligi ya kwanza Afrika kucheza kwa Teknolojia ya usaidizi wa Video kwa waamuzi ‘VAR’.

Batola Pro, imekuwa Ligi Kuu ya Kwanza barani Afrika  kutumika VAR na mchezo wa kwanza ulikuwa Ijumaa kati ya IRT Tangier walioibuka  ushindi  wa  mabao  2-1 dhidi ya  FUS Rabat.

Msuva ambaye aliiongoza Difaa, Jumamosi katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi hiyo, amesema kitu muhimu zaidi kwake ni ushindi ambao wameupata   wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Mohammed V Athletic Complex dhidi ya Wydad Athletic Club.

“Tumeanza vizuri mzunguko wa pili ambao siku zote huwa mgumu kutokana na umhimu wake kwa kila timu, mchezo ulikuwa mgumu lakini kucheza kwetu kwa kushirikiana kulitusaidia kupata bao. VAR ilikuwepo ni jambo zuri kuwa sehemu ya historia.

“Lakini ingekuwa historia isiyo na maana kwangu kama tungepoteza huo mchezo. Sina tatizo na VAR ila nilitoa tahadhari ili isijekuleta shida maana Afrika ni tofauti na Ulaya,” alisema Msuva.

Kiujumla mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kukumbana na VAR ni nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akiwa na klabu yake ya KRC Genk katika mashindano mbalimbali ya ushindani barani Ulaya.

Licha ya kuwa Morocco ndio taifa la kwanza kuanza kutumia VAR katika Ligi yao ya ndani Msuva alikumbana na teknolojia hiyo kwa mara ya kwanza wakati wa fainali za mataifa ya Afrika nchini Misri.