Msuva amaliza tetesi akitua Wydad Casablanca
Muktasari:
Taarifa hizi mpya zinakatisha sintofahamu zilizokuwepo kuhusu usajili wa nyota huyo kwenye klabu mbalimbali alizokuwa akihusishwa nazo kama Benfica ya Ureno.
WAKATI akiwa nchini Uturuki kwenye kambi ya timu ya Taifa Stars, inayoajiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Tunisia, Winga mshambuliaji Simon msuva, ametajwa kusaini mkataba kuichezea timu ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Taifa Stars itacheza na Tunisia Ijumaa hii Novemba 13 na baada ya hapo itawasubiri wapinzani wao hao kwenye mchezo wa pili utakaochezwa Novemba 17 jijini Dar es Salaam.
Wydad ambayo ni miongoni mwa timu kubwa zenye mafanikio nchini kwao Morocco huku ikiwa na mwendelezo bora wa kufanya vema kwenye ligi ya mabingwa Afrika.
Wydad msimu uliopita ilicheza fainali ya ligi ya mabingwa dhidi ya Esperance ya Tunisia, ambapo usajili wa Msuva utakuwa na lengo la kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.
Msuva ambaye amemaliza mkataba wake na timu yake ya Hassania El Jadida ya pale pale Morocco, anatajwa kusaini mkataba wa miaka minne kuitumikia Wydad Casablanca.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Kanda ya Kaskazini, Jalal Bouonouar, usajili wa Msuva kwa Wydad ni kati ya usajili mkubwa kwenye ligi kuu ya nchini humo, Botola Pro.
Endapo Msuva atajiunga na timu hiyo, atakuwa ameondoka ndani ya timu yake ya Hassania El Jadida iliyomfungulia njia na atamuacha nyota mwenzake Hassan Kibabage kubaki kuitumikia timu hiyo.