Msuva aipeleka Difaa nusu fainali ya kombe la mfalme

Muktasari:

  • Msuva alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili kabla ya kutimikia Difaa

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Saimon Msuva ameivusha timu yake ya Difaa El-Jadida kucheza hatua nusu fainali ya Kombe la Mfalme, Morocco (Throne Cup) kutegeneza mabao yaliyoipa ushindi wa 2-0 dhidi Chabab Rif Hoceima.

Katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza  Difaa ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 na wenyeji wao, Chabab Rif Hoceima.

Matumaini ya Difaa kutinga hatua ya nusu  fainali yaliibuka dakika ya 64 wakati Msuva akitokea pembeni na kupiga klosi iliyomkuta Adnane El Ouardy aliyefunga bao la kwanza kabla ya Mtanzania huyo kuchangia kupatikana kwa bao la pili dakika ya 89, lililofungwa na Hamid Ahadad.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Msuva alisema kupindua kwao matokeo kumechangiwa na hamasa za mashabiki wao ambao muda wote wa mchezo walikuwa wakiwashangilia.

"Hawakuwa wamekaa kwenye viti vyao, karibu muda wote wa mchezo walikuwa wanatoa hamasa kwetu kwa kuimba nyimbo mbalimbali za kiarabu." alisema Msuva moja kwa moja kutoka El Jadida.