Msonda gari limewaka, mjipange
STRAIKA mpya wa Yanga, Kennedy Musonda mwishoni mwa wiki alifunga mabao mawili wakati timu hiyo ikiifumua Rhino Rangers kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC) 7-0 na sasa ametuma salamu nzito kwa wapinzani katika Ligi Kuu Bara akisema gari sasa limewaka.
Musonda aliyefunga mabao hayo yakiwa ya kwanza kwake katika mechi za mashindano alisema alikuwa katika presha kubwa kabla ya kufunga, lakini sasa anajiona yuko huru.
Nyota huyo kutoka Zambia alisema baada ya mabao hayo anajiona yuko katika hali ya kujiamini zaidi kufunga zaidi katika mechi zinazofuata za timu yake. Yanga inaikaribisha Namungo katika mechi ya Ligi Kuu Bara wikiendi hii kabla ya kusafiri kwenda Tunisia kwa mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir ambako Kocha Nabi Mohammed amepania kuanza kwa kishindo.
“Mimi ni mshambuliaji kitu kikubwa kwangu ni kuisaidia timu kupata ushindi, kawaida usipofunga kuna presha inakuja lakini niliamini nitafunga,”alisema Musonda aliyetua Jangwani akiwa ametoka kufunga mabao 11 na kuwa kinara wa wafungaji wa Ligi Kuu ya Zambia. “Presha sasa imeondoka niko huru, hali ya kijiamini imerudi tena nimefunga wakati timu ikishinda vizuri, sasa kazi ni moja kumuomba Mungu ili nifunge zaidi katika mechi zinazofuata,” aliongeza Musonda aliyekuwa amefunga mabao mawili akiwa na uzi wa Yanga kwenye michezo ya kirafiki.
Aidha Musonda alisema anajivunia jinsi ushirikiano ulivyo ndani ya kikosi hicho tangu alipofika akisema anaona matokeo zaidi mazuri yatakuja kwa timu yake.
“Tunacheza kwa ushirikiano sana kuanzia uwanjani na hata tunapokuwa kambini na mazoezini, tupo kifamilia zaidi ndio maana hata uwanjani mambo yamekuwa rahisi, kitu muhimu ni ushindi wa timu na naona tutafanikiwa zaidi kushinda mechi zijazo.”