Msako wa tiketi ya CAF
Muktasari:
- KMC ndiyo imeondoshwa mapema baada ya kufungwa kwa penalti 3-2 dhidi ya Bandari Tanzania inayoshiriki First League. Dakika tisini za mechi hiyo zilimalizika kwa sare ya 3-3, ndipo penalti zikaamua mshindi.
WIKIENDI hii hatua ya 32 Bora katika Kombe la Shirikisho (FA) inakwenda kuchezwa baada ya ile ya 64 kumalizika huku tukishuhudia timu moja kati ya 16 za Ligi Kuu Bara ikitoka mapema.
KMC ndiyo imeondoshwa mapema baada ya kufungwa kwa penalti 3-2 dhidi ya Bandari Tanzania inayoshiriki First League. Dakika tisini za mechi hiyo zilimalizika kwa sare ya 3-3, ndipo penalti zikaamua mshindi.
Fursa ya bingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, imetajwa kuongeza ugumu na ushindani mkali wa hatua ya 32 bora, mechi zinazotarajiwa kuchezwa Machi 6 hadi 8, 2026.
Michuano hii imekuwa na mvuto wa aina yake tangu kuanzishwa mwaka 1967 kipindi cha FAT ambapo 2003 hadi 2015 ikasimama, na kuendelea msimu wa 2015-2016 ilipokuja kupata udhamini kutoka Azam Media uliodumu hadi 2022-2023, kisha 2023-2024 ni zama za CRDB Bank ndiyo tupo sasa.
Tangu kureje kwa mashindano hayo msimu wa 2015-2016, Yanga imekuwa bingwa mara nyingi ikibeba taji hilo misimu mitano kati ya kumi ambayo ni 2015-2016, 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025. Timu zingine zilizobeba taji kipindi hicho ni Simba (2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021), Mtibwa Sugar (2017-2018) na Azam (2018-2019).
ZINAZOSHINDANA
Katika hatua ya 32 Bora, Ligi Kuu Bara imeingiza timu 15 ambazo ni TRA United, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, JKT Tanzania, Pamba Jiji,
Mashujaa, Simba, Namungo, Mbeya City, Fountain Gate, Mtibwa Sugar, Azam, Singida Black Stars, Coastal Union na Yanga.
Upande wa Ligi ya Championship zipo 14 baada ya mbili kuondoshwa, Barberian na Bigman.
Timu zilizobaki ni Kagera Sugar, Geita Gold, Mbeya Kwanza, Transit Camp, Polisi Tanzania, Mbuni, Kengold, Songea United, TMA Stars, Stand United, Gunners, B19, Hausang na African Sports.
Kwa upande wa First League, ipo moja ambayo ni Bandari Tanzania kama ilivyo Ligi ya Mabingwa ikiwakilishwa na Kijiwe Nongwa, huku Nyika ikitokea Ligi Daraja la Tatu Pwani.
RATIBA ILIVYO
Katika hatua ya 32 bora, Azam iliyoiondosha Endumenti kwa bao 1-0, inakwenda kucheza dhidi ya Mbeya Kwanza ambayo nayo iliifunga FGA Talents mabao 5-0, huku mabingwa watetezi Yanga waliyoichapa Cosmopolitan mabao 2-0, wamepangwa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania iliyofuzu baada ya wapinzani wake THB kushindwa kutokea uwanjani.
Simba ambayo iliifunga Greenland mabao 3-0, itacheza dhidi ya B19 FC iliyoitoa Dhujau kwa mabao 7-0, wakati Singida Black Stars iliyofuzu kwa kuifunga Copco mabao 3-1, imepangwa kukabiliana na Songea United iliyoiondosha Vijana kwa mabao 2-1.
Mechi zingine ni; Geita Gold vs Nyika, JKT Tanzania vs Hausang, Coastal Union vs Stand United, Namungo vs Kagera Sugar, Mbeya City vs Bandari Tanzania, Fountain Gate vs Gunners, TRA United vs Kijiwe Nongwa, Tanzania Prisons vs TMA Stars, Dodoma Jiji vs African Sports, Pamba Jiji vs Transit Camp, Mtibwa Sugar vs Mbuni na Mashujaa vs KenGold.
Katika upangaji wa droo hiyo, pia ilipangwa itakavyokuwa hatua ya 16 bora, ambapo mechi zake zinatarajiwa kuchezwa kuanzia Aprili 9 hadi 11 mwaka huu.
HATUA YA 16 BORA
Baada ya kumalizika 32 Bora, itafuata 16 Bora ambayo kwa misimu mingi, imekuwa ikizihusisha timu nyingi za Ligi Kuu Bara kwani ndiyo huwa zinafanya vizuri kwa kiasi kikubwa kutokana na huko nyuma kucheza na timu za madaraja ya chini.
Ukiangalia kwa sasa timu 32 zilizobaki, 15 ni za Ligi Kuu Bara ambazo ratiba yake inaonyesha moja inacheza dhidi ya timu kutoka First League ambapo ni Mbeya City vs Bandari Tanzania, huku TRA United dhidi ya Kijiwe Nongwa inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Mkoa. Zilizobaki ni timu za Ligi Kuu dhidi ya Championship.
Itakayoshinda kati ya Singida Black Stars dhidi ya Songea United, itacheza na mshindi baina ya Mbeya City dhidi ya Bandari Tanzania, huku mshindi kati ya Azam dhidi ya Mbeya Kwanza, mpinzani wake ni mshindi baina ya Fountain Gate dhidi ya Gunners.
Mshindi kati ya Yanga dhidi ya Polisi Tanzania, atacheza na Tanzania Prisons au TMA Stars, huku pia mshindi kati ya Simba dhidi ya B19FC, mpinzani wake ni Dodoma Jiji au African Sports.
Zingine zitakuwa hivi; Namungo/Kagera Sugar vs TRA United/Kijiwe Nongwa, Coastal Union/Stand United vs Pamba Jiji/Transit Camp, JKT Tanzania/Hausang vs Mtibwa Sugar/Mbuni na Geita Gold/Nyika vs Mashujaa/Ken Gold.