Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeya City mguu mmoja Ligi Kuu, Prisons ni maajabu tu zikisubiriwa dakika 90

MBEYA Pict

Muktasari:

  • Mshindi wa jumla katika mechi mbili atabaki Ligi Kuu huku atakayepoteza akikutana na Polisi Tanzania ya Championship kujiuliza hatma yake. 

Mabao ya Said Naushad na Hijja Shamte yametosha kuiweka mazingira mazuri Mbeya City kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa mtoano 'Play Off' mkondo wa kwanza uliochezwa leo Julai 5, 2026 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Hata hivyo, Prisons itajilaumu kwa kukosa penati kupitia straika wake Jeremia Juma baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa Soud Dondola. 

Kufuatia matokeo hayo, timu hizo zimebakiza dakika 90 za mwisho katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Julai 8, 2026 uwanjani hapo ambapo Prisons itakuwa mwenyeji kujua hatma ya nani kubaki Ligi Kuu. 

Baada ya matokeo ya jumla kwa mechi hizo, timu itakayopoteza itakutana na Polisi Tanzania ya Championship iliyofuzu kufuatia ushindi wa jumla wa mabao 7-0 dhidi ya Mbeya Kwanza. 

Katika mchezo wa leo, Mbeya City ikiwa mwenyeji imetumia vyema nafasi ilizopata na kufanikiwa kuanza vyema play off hiyo. 

Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu ilianza kupata bao dakika ya 17 kupitia kwa Naushad kabla ya Shamte kuzamisha jahazi la Maafande hao wa Magereza dakika ya 89 na kuzima shangwe la wapinzani wao. 

Timu hizo za jijini Mbeya, zimeangukia mtoano baada ya Prisons kumaliza nafasi ya 13 kwa pointi 32 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC 2025-2026, huku City ikiwa ya 14 kwa pointi 30 na sasa zinajiuliza kupitia mchujo huo. 

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shedrack Nsajigwa amekiri matokeo hayo kutokuwa mazuri kwake akieleza kuwa mpira una maajabu na hawajakata tamaa wakisubiri marudiano. 

"Tuwapongeze Mbeya City kwa matokeo japokuwa tulipaswa kumaliza angalau kwa sare kwa kuwa hatujazidiwa sana, mabao mawili ni mengi ila tunasubiri mechi ya mwisho kujua hatma yetu," amesema Nsajigwa. 

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga amesema mwanzo huo si mbaya kwao japo hawawezi kujiaminisha zaidi kuwa salama, akiahidi kuwa nguvu waliyotumia leo ndio hiyo hiyo ya mechi ijayo. 

"Tunaenda kujipanga kwa nidhamu na mechi ijayo, tutawaandaa vyema wachezaji ndani na nje ya uwanja kuhakikisha tunalinda ushindi huu na kubaki salama Ligi Kuu," amesema kocha huyo.