MPAKA HOME : Kwa Dante ni kazi tu!

Beki wa kati wa Mtibwa Sugar Andrew Vicent 'Dante'.
Muktasari:
Dante ni yule beki wa kati anayevaa jezi namba 12, kichwani amefuga nywele kwa mtindo wa rasta na katika mechi yao ya mwisho Uwanja wa Taifa, alihakikisha mkali wa Yanga, Mzimbabwe Donaldo Ngoma hatambi.
ILIKUWA safari ndefu kiasi hadi kufika mahali ambapo anakaa beki wa kati wa Mtibwa Sugar, Andrew Vincent ‘Dante’. Lengo la kumuibukia maskani yake ni kutaka kukupa aina ya maisha yake nje ya soka.
Dante ni yule beki wa kati anayevaa jezi namba 12, kichwani amefuga nywele kwa mtindo wa rasta na katika mechi yao ya mwisho Uwanja wa Taifa, alihakikisha mkali wa Yanga, Mzimbabwe Donaldo Ngoma hatambi.
Anakaa Kingugi, Mbagala Kiburugwa, jijini Dar es Salaam pamoja na wazazi wake, baba yake, Vincent Chikupe na mama Faustina Vincent, sambamba na ndugu zake Geofrey, Doris, Baraka, Severa pamoja na mjomba wake, John Lusambo. Wote kwa pamoja walimkaribisha mwandishi wa kona hii kwa bashasha kubwa kupindukia.
Lakini siri moja ni kwamba, ukifika nyumbani kwao, bila taarifa huwezi kuingia kwa sababu kuna ulinzi wa maana, wana Mbwa wakubwa wa kisasa (German Shepherd Dog) sita, mbali na vitoto wadogo ambao wanatunzwa katika chumba maalum, sasa ukikosea kidogo tu, usishangae kugeuzwa kitoweo.
Kinachovutia zaidi ni namna wanavyoishi, mbali na maisha ya soka, wazazi wake wamekuwa mstari wa mbele kumfundisha namna ya kutafuta pesa kwa kutumia ujasiriamali nje ya soka.
Familia hiyo imejikita kwenye shughuli za kilimo na ufugaji, hapo nyumbani kwao kuna bustani ya chakula mbalimbli kama Migomba ya Ndizi, mboga za majani, pia ni wakifuga Ng’ombe wa maziwa, Mbuzi na Kuku. Yaani kwao ni kazitu.
Dante aliyesoma Shule ya Msingi Barracks na kumalizia darasa la saba, Kingugi ana elimu ya Sekondari aliyoipata Shule ya Deblabant.
Awali wazazi wake hawakumruhusu kucheza soka wakitaka kwanza asome, lakini wakajikuta wanakubaliana naye waliposhtukia tayari amejitosa kitambo na kutesa.
Hata hivyo, pamoja na ‘kumpiga biti’ hilo, kumbe kipaji hicho ni urithi kutoka kwa baba aliyekipiga klabu ya Polisi Rukwa Daraja la Kwanza miaka ya nyuma. Na soka ndiyo ilimbeba akapata ajira ya askari mara tu aliposajiwa na Polisi Rukwa iliyomnyakua kutoka na Chanji ya Sumbawanga.
NYUMBANI
Mwanaspoti: Hodi!
Dante: Karibu hapa ndiyo nyumbani kama unavyotuona, huyu ni mama yangu, wadogo zangu na anko (anawatambulisha).
Mwanaspoti: Unapokuwa hapa nyumbani unapendelea kujishughulisha na nini, na unapojipunzisha ni burudani gani unayoipendelea?
Dante: Ninapokuwa hapa nyumbani, nafanya shughuli zote za nyumbani licha ya kuwa wapo wadogo zangu kwa sababu napenda kujishughulisha, nafua, nasafisha nyumba, nafanya usafi na pale nje umeona kuna mifugo, ninapokuwa hapa mimi ndiyo nahakikisha wamekula, usafi na mambo mengine yote. Wazazi wangu wamenifundisha hivyo tangu mdogo, hivyo kwangu ni kama kawaida, sioni tabu na hata nikiwa na maisha yangu mwenyewe hapo baadaye hata kama sitakuwa nacheza mpira, siwezi kutetereka kwa sababu naujua vizuri ujasiriamali.
Na ninapomaliza shughuli zangu, muda mwingi nakuwa na Play Station, hapo nacheza ‘game’ mbalimbali, pia napenda kuangalia soka hasa la Hispania, ligi ya hapa nyumbani na marudio ya mechi zetu, ninaporudia ndiyo najua mapungufu yangu na kurekebisha makosa kupitia televisheni.
MAHUSIANO
Mwanaspoti: Vipi unaye mchumba?
Dante: Ndiyo ninaye mchumba na nampenda sana anaitwa, Cecy George anaishi Nzasa hapa hapa Dar es Salaam.
Mwanaspoti: Mlikutana katika mazingira gani na mna muda gani?
Dante: Kusema kweli hatuna muda mrefu sana, tangu tumeanzisha mahusiano ni kama mwaka hivi, lakini ni mtu ambaye nilikuwa namfahamu kwa muda mrefu, lakini siku ambayo nilipata nafasi ya kumfikishia ujumbe wangu kuwa nampenda. Nakumbuka ilikuwa kule kwenye ufukwe wa Jiji, nikwenda na mambo yangu na yeye alikuwa na yake pamoja na rafiki zake.
Mwanaspoti: Kitu gani kilichokushawishi ukampenda na malengo yenu ni nini?
Dante: Kikubwa ni tabia yake, kama nilivyokwambia ni msichana ambaye nilikuwa namfahamu kwa muda mrefu, mstaarabu, anajiheshimu na anajua maisha. Kwake napenda kila kitu na kimwonekano ni mrembo, sura yake na tabasamu ndiyo linalonivutia zaidi.
Nina malengo naye, nataka hapo baadaye aje kuwa mke wangu na mama wa watoto wangu na kwa sababu sina malengo naye mabaya, nimeshamleta hapa nyumbani.
MAMA ATOA LA MOYONI
Mwanaspoti: Dante ni mtoto wa aina gani na unafurahia anavyocheza mpira?
Mama Dante: Kwa kweli namshukuru Mungu kwa sababu ni kijana msikivu na hata anapokuwa hapa nyumbani tunafurahi kwa sababu tunajua msaada umefika. Anapokuwa hapa anasaidia usafi na kule kwenye mifugo yeye ndiyo hufanya kila kitu, na anapomaliza majukumu yake ya uwanjani muda wake mwingi anapenda kuutumia hapa kwenye televisheni.
Kuhusu kucheza soka kweli namshukuru na namwombea kwa Mungu ndoto zake zifanikiwe kwa sababu ni kitu ambacho alikipenda tangu alipokuwa mdogo. Unajua mwanzoni tulimkataza kwa sababu tulipenda asome, lakini alipomaliza kidato cha nne tukashtukia tu amechukuliwa na timu hukoo. Napenda maendeleo yake na nafurahi sana ninapomwona uwanjani anacheza.