Morrison, Mugalu gumzo kila kona

MASHABIKI wa soka jijini hapa wanazungumzia zaidi uwepo wa Bernard Morrison na Chris Mugalu kwenye kikosi cha Simba kitakachowavaa AS Vita Ijumaa saa 3 usiku.
Simba imetua Kinshasa na wachezaji 27 ili kujiweka tayari kwa lolote linaloweza kutokea hata kama baadhi yao watakumbana na mizengwe ya ugonjwa wowote.

Kwa mujibu wa mchambuzi na mtangazaji mahiri wa michezo kwenye redio maarufu ya Top Congo FM, Jenovic Mbowa wachezaji hao wawili ndio wanaosemwa sana na wanapewa nafasi kubwa ya kusumbua kwa vile wanaielewa vizuri DR Congo na aina ya soka na mambo ya ndani na nje ya uwanja.
Alisema Morrison kama akiongeza umakini kwenye kufunga ndiye anayeweza kuwa na madhara zaidi ndani katika mechi hiyo kwa vile wanamjua.
“Mugalu ni mchezaji mzuri na isitoshe ni Mkongo, anaelewa mambo mengi ya hapa kwa vile alicheza sana FC Lupopo ya Lubumbashi anawajua sana Vita, atasumbua,” alisema
“Morrison ni Mghana, lakini amecheza hapa sana anajua ujanja wote ndiyo maana wanamhofia, alicheza AS Vita baadae akaenda Motema Pembe. Ni mchezaji msumbufu sana na wanamjua, hivyo akiongeza makali yake kidogo tu ana uwezo wa kufanya vizuri kwenye mchezo huo.
“Morrison anaujua sana uwanja wa Martyrs ambako hii mechi itapigwa, kwa hiyo itakuwa faida kubwa sana kwake kuamua huu mchezo ingawa sijajua kiwango chake kitakuwaje siku hiyo,” aliongeza Jenovic ambaye ni mmoja wa wachambuzi wanaoheshimika zaidi Kinshasa kutokana na ukubwa wa kituo chao.
Kuhusu AS Vita alisema wanaendelea kujinoa ingawa baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye timu ya Taifa wamechelewa kujiunga na wenzao kambini ila bado anawapa nafasi ya kufanya vizuri haswa kwa kuangalia rekodi zao za ligi ya ndani na kimataifa katika uwanja huo.
SIMBA KUWAKOSA MASTAA WATATU
Wakati huo huo, Wekundu wa Msimbazi itawakosa nyota wake watatu kwenye mchezo huo wa Ijumaa.
John Bocco ana jeraha la goti, huku Perfect Chikwende ambaye aliichezea FC Platinam kwenye mchezo wa awali wa michuano hiyo na David Kameta ‘Duchu’ akiwa na majukumu ya timu ya taifa chini ya miaka 20 inayokwenda kwenye fainali za Afcon chini ya miaka 20 za nchini Mauritania kuanzia mwezi huu.