Morrison apewa mazoezi Yanga

Friday June 24 2022
Morrrison PIC
By Mwandishi Wetu

MABOSI wa Yanga wameshusha pumzi baada ya kusikia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limesogeza mbele muda wa kuanza mashindano yake kwa ngazi ya klabu, lakini taarifa hizo zikafungua milango za usajili wa winga Bernard Morrison aliyepewa ratiba ya kujifua akiwa Ghana.

Yanga ina uhakika sasa kwamba itakuwa na winga huyo aliyekuwa akikipiga Simba msimu huu atavaa uzi wa njano na kijani kwa msimu ujao na haraka imemtumia programu maalumu ya kuanza kumuandaa kwa mazoezi akiwa kwao.

Usajili wa Morrison ndani ya Yanga umepigiwa tiki na makocha ingawa wanapigania usajili wa Simon Msuva kama chaguo la kwanza kwenye nafasi hiyo. Mwanaspoti linafahamu kuwa, Morrison aliyepo Ghana kwa mapumziko tayari ameshakubali kuja kusaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga akirejea klabu hiyo ambayo ndiyo iliyomleta nchini kabla ya kutimkia Simba katika usajili uliolalamikiwa na Yanga hadi kukimbilia Fifa kushtaki.

Katika programu hiyo Morrison anatakiwa kuifuata kwa umakini kuanza kujifua mapema kabla ya kurejea nchini kuungana na wenzake tayari kwa safari ya Uturuki kwenye maandalizi ya msimu. Makocha hao wamempiga mkwara kwamba kama hatafuata ratiba hiyo ataumbuka atakapotua nchini ambapo akili kubwa ni kutaka winga huyo asiongezeke uzito wa mwili wakati huu akiwa kwao.

“Wamembana sana (Morrison) makocha wanasema kama kupumzika muda umeshatosha, lakini sasa ni lazima afanye mazoezi haya kila siku ili kusudi atakapokuja kuungana na wenzake asiwe na uzito mkubwa ambao utamchelewesha kuwa katika kiwango bora,” alisema mmoja wa bosi wa klabu hiyo.

“Unajua hapa katikati tulianza kupata wasiwasi wa kumsajili kutokana na suala la mkataba wake, lakini sasa tuna uhakika tutakuwa naye kwa msimu ujao,” aliongeza bosi huyo.

Advertisement

Mkataba wa Morrison na Simba ulikuwa unafikia tamati Agosti 14, ambapo kwa ratiba ya awali Yanga walikuwa katika wakati mgumu kutokana na kalenda ya awali ya mashindano ya CAF kuonyesha msimu mpya ungeanza wiki ya pili ya Agosti.

Hata hivyo, CAF wiki hii walibadilisha kalenda hiyo na kuonyesha msimu mpya sasa utaanza wiki ya kwanza Septemba hatua ambayo itaifungulia Yanga milango ya kumsajili Morrison.

Mapema Simba ilionekana kama kutaka chochote Yanga ikimwambia winga huyo aliyeomba barua ya kuwa huru, ikimtaka kusubiri hadi mkataba wake umalizike hatua ambayo ingemweka katika wakati mgumu raia huyo wa Ghana kuwahi mashindano ya CAF.

Yanga sasa itakuwa huru kumsajili Morrison Agosti 15 siku ya mwisho ya usajili wa CAF ikiwa ni siku moja baada ya winga huyo mkataba wake kufikia tamati na Simba. Yanga imepania kurudi kwa nguvu kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.

Advertisement